Tanzania na Afrika Kusini zimekubaliana kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kukuza Ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) na Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini Mhe. Ronald Lamola uliofanyika katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah, Balozi wa Tanzania Afrika Kusini Mhe. James Bwana, Balozi wa Afrika Kusini nchini Mhe. Noluthandi Mayende-Malepe pamoja na Maafisa wengine Waandamizi kutoka Tanzania na Afrika Kusini.
Katika kikao hicho Tanzania na Afrika Kusini zimekubaliana kuendelea kufanya kazi kwa pamoja katika nyanja mbalimbali na pia kufanya majadiliano ya mara kwa mara ili kutatua changamoto zinazozuia kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya pande mbili.
Akizungumza katika Kikao hicho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Kombo ameeleza utayari wa Tanzania kuendelea kushirikiana na Afrika Kusini na kufanya shughuli za Biashara na Kilimo kati yao kuendelea kuimarisha ushirikiano na hivyo kuzinufaisha nchi zote mbili.
“Napenda kuthibitisha dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuimarisha ushirikiano wa uwili hasa katika eneo la kukuza ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote. Kwa kudumisha, kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wetu wa muda mrefu, tunaweza kufanikisha mafanikio makubwa zaidi”. Alisisitiza Mhe. Waziri Kombo.
Ametoa wito kwa watendaji wa Tanzania kushirikiana na watendaji wa Afrika Kusini ili kufanya kazi kwa karibu na kwa pamoja ili kuendelea kushirikiana kiuchumi.
Naye Waziri wa Afrika Kusini Mhe. Lamola ameeleza kuwa Afrika Kusini itahakikisha makubaliano yaliyosainiwa yanatekelezwa kwa kuandaliwa Mpango wa Utekelezaji na Ufuatiliaji.
Halikadhalika, amezisihi Mamlaka za nchi zetu kujadiliana na kukamilisha michakato ya utiaji saini wa Makubaliano na Mikataba katika sekta mbalimbali ili kuimarisha ushirikiano wao na Tanzania.
“Ni muhimu kuanzisha utaratibu wa ufuatiliaji ili kushughulikia masuala tuliyokubaliana kwa ufanisi.
Afrika Kusini itahakikisha watendaji wake wanashirikiana na upande wa Tanzania na kufanyia kazi masuala yote yenye changamoto kwa lengo la kuyatatua kwa pamoja ili kuendelea kukuza Ushirikiano wetu wa kiuchumi na Tanzania”, alisema Mhe. Lamola.
Amewahimiza wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini kushiriki kwa wingi katika shughuli za biashara na uwekezaji ambazo zimekuwa zikifanyika kwa manufaa ya pande zote.
Ameongeza kuwa Maafisa kutoka pande zote mbili wataendelea kushirikiana kwa karibu na kuweka mazingira bora ya biashara kwa manufaa kwa nchi na watu wake.
No comments:
Post a Comment