Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi wa Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Kati pamoja na kamati za siasa za jimbo na wadi alipofanya ziara ya kuimarisha chama Wilayani humo katika Ukumbi wa kituo cha Walimu (TC) Dunga.
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amewaagiza viongozi na wajumbe wa vikao vya maamuzi vya kuwapitisha wagombea watakao peperusha bendera ya CCM kutenda haki katika maamuzi yao.
Mjumbe huyo ameyaeleza hayo akiwa kwenye ziara yake ya kichama yenye lengo la kuimarisha chama cha Mapinduzi iliyoanzia katika wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo alizungumza na viongozi wa halmashauri kuu ya wilaya, kamati za siasa za jimbo na wadi, katika ukumbi wa kituo cha Walimu (TC) Dunga.
Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa viongozi na wajumbe wa vikao hivyo kusimamia haki kwa wagombea waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama hicho na kutokupokea rushwa ya aina yoyote ile jambo ambalo litaepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Mhe. Hemed amewahimiza viongozi na wajumbe hao wa kamati hizo, kuhakikisha wanatumia nafasi zao vyema kwa kupendekeza wagombea wa CCM wenye sifa, wanaokubalika katika jamii hatua ambayo itarahisha ushindi wa kishindo.
Katika hatua nyengine, Mhe. Hemed amesema huu ni wakati muhimu zaidi kwa viongozi na wanachama wa CCM kuhakikisha wanaongeza ushirikiano na kufanyakazi kwa karibu, hasa ikizingatiwa chama hicho kipo kwenye maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.
Amebainisha kuwa ni wajibu wa kila kiongozi wa chama kwa nafasi yake, wanachama na washabiki wa chama hicho, kuhakikisha wanakipambania chama ili kiweze kuibuka na ushindi wa kishindo kwenye mkuu.
Ameeleza huu si wakati kwa viongozi na wanachama wa CCM kukaribisha mitafaruku na migongano baina yao, bali ni wakati wa kuongeza mshikamano utakaokiwezesha chama kupata ushindi wa kuongoza dola.
Aidha Mhe. Hemed alifahamisha kuwa ndani ya CCM wanachama wote wana haki sawa, hivyo amewataka wanachama wenye sifa ya kugombea wakati utakapofika kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu na kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.
Amewataka wanachama wa CCM kuacha makundi na matabaka ndani ya chama hasa baada ya mchakato wa kupitisha wagombea na badala yake wazidi kuungana katika Kuimarisha chama na kuwapa ushirikiano wagombea watakaoteuliwa kugmbea kwa tiketi ya CCM.
Kwa upande wake katibu wa Idara Maalum ya Siasa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, Ndugu Khamis Mbeto, amewaasa wanachama wa CCM katika kuelekea uchaguzi wa kura za maoni kujiepusha na makundi hasa baada ya uchaguzi jambo ambalo linaweza kuleta taswira mbaya ndani ya chama.
Mbeto aliwahakikishia wanachama wa CCM kuwa kamati ya kuteua wagombea itafanya kazi kwa kufuata miongozo na kutenda haki na kila anaestahiki na mwenye sifa atapatiwa haki yake.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Kati, Omar Discus Moris amesema wilaya hiyo inaendelea na zoezi la uhakiki wa wanachama jambo ambalo litawahakikishia kupata kadi za kielektroniki.
Moris alisema viongozi wa wilaya ya Kati wamejipanga kuendelea kusajili wanachama wapya ambapo hivi karibuni wamesajili zaidi ya wanachama elfu mbili jambo ambalo linaamsha ari na hamasa kwa Wilaya hiyo kuendelee kuwa ngome Imara ya Chama cha Mapinduzi.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 10.06.2025.
No comments:
Post a Comment