Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Ndg. Stephen Wasira akizungumza na Wanachama pamoja na viongozi mbalimbali wa CCM Wilaya ya Tunduru, Leo Juni 10, 2025 akiwa Katika Tiara make ya kukagua Uhai wa Chama Mkoa wa Songea.
*Ataja sababu za ‘Oktoba Tunatiki’ kwa Dk. Samia, Dk. Nchimbi*Asema kaulimbiu ‘No Reform No Election’ inaelekea mwisho
*Asema Watanzania hawana historia wala sababu Wakristo, Waislamu kugombana
*Awahakikishia wananchi uchaguzi uko pale pale, amani nchini uhakika
Na Mwandishi Wetu, Tunduru
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Stephen Wasira, amewataka Watanzania wakiwemo wanachama na wapenzi wa Chama kujiandaa kwenda ‘kutiki’ kwa kumpigia kura Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan na Mgombea Mwenza Dk. Emmenuel Nchimbi katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Amesisitiza kuwa, hakuna mtu au kikundi cha kuzuia uchaguzi huku akiwataka wananchi kutobabaishwa na kaulimbiu ya ‘No Reform No Election’ ya Chama cha CHADEMA kwa kuwa inakwenda kufikia mwisho kwa kuwa tayari CCM na wanachama wake wamejiandaa kutiki kwa Dk. Samia Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na wana CCM, wananchi, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kijamii alipokuwa katika kikao cha ndani wilayani Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, Wasira alieleza hatua kwa hatua sababu ambazo zinakifanya Chama na Watanzania wengine kumpigia kura Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza wake Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CCM.
“Usibabaishwe na maneno hakuna mtu wa kuzuia uchaguzi, utakuwepo na ninyi mabalozi toweni watu wetu waende wakapige kura muda ukifika, waende ‘wakatiki’ na tiki yenyewe ni rahisi maana unaona CCM na alama ya jembe na nyundo.
“…Utamuona mgombea wetu Dk. Samia Suluhu Hassan, utamuona Dk. Emmanuel Nchimbi halafu mbele ya hao watu unaweka tiki. Kwa hiyo nilitaka niwaeleze haya mambo muyajue vizuri ili msije kubabaishwa.” Alieleza.
MIAKA MINNE NA MARIDHIANO
Akieleza zaidi Wasira alisema miaka minne iliyopita Rais Samia alipoingia madarakani aliamua kuja na mfumo wa maridhiano na kupitia maridhiano kuna mambo mengi ya msingi yamefanyika.
Kwa mujibu wa Wasira, vyama vya siasa 18 ambavyo vinatambuliwa na msajili wa vyama vya siasa nchini vilishiriki vikao mbalimbali lakini CHADEMA walitaka wasikilizwe peke yao, Rais Samia alikubali na wakasikilizwa.
“Kwa hiyo hakuna uwezekano wowote kwa kuzingatia Katiba na sheria za Tanzania ambao unaweza kusema uchaguzi utaahairishwa, nawaambia haya kwa sababu ninyi ni viongozi wa watu...
“Hii kaulimbiu ya ‘No Rerfom No Election’ isiwazuie kulima korosho, isiwazuie kupiga salfa. Hamna kitu hapa ninyi endeleeni kwenda kujiandikisha, narudia hii kaulimbiu mwisho wake unakaribia kwa sabababu hata juzi Katibu Mkuu wa CHADEMA (John Mnyika) alikuwa Kondoa…
“Akaenda akawaambia wananchi ‘no reform no election’ wakamwambia sisi tunaenda kupiga kura…tena walimwambia macho macho tunaenda kutiki Okotba. Tena tiki kubwa kabisa.
“Nimewaeleza yanayojiri ili muwe na elimu ya kupambana na uongo, maana uongo unafanana na giza na ukweli unaogopwa na uongo kama giza livayoogopa umeme. Umeme, giza katika umeme linatoweka kama halikuwepo, kwa hiyo chama chetu kinajiandaa kwa uchaguzi,” alisisitiza.
AMANI, UMOJA, MSHIKAMANO
Kuhusu amani, umoja na mshikamano, Wasira aliwahakikishia wananchi kuwa nchi iko salama huku akitumia nafasi hiyo kusisitiza kwamba Tanzania hakuna kubaguana kwa dini, rangi wala kabila.
Wasira alisema hata katika dini hakuna ubaguzi na hakuna wanaoweza kugombana kwa sababu ya dini iwe Waislamu au Wakristo.
“Sasa watu wa dini mbili wanaweza kugombana kwa sababu gani, tumesema kila mtu anasali na hakuna anayezuiwa. Ukienda msikitini hakuna aneyezuia, ukienda kanisa hakuna aliyezuiliwa wala kuulizwa. Tena ukiuliza ndugu zangu wa Kiislamu na ukiuliza Wakristo wote watakwambia chimbuko la dini zao ni Ibhrahimu, sasa Ibrahim kasema mgombane?
“Sisi wote chimbuko moja tena mimi si msomi wa Koraan lakini ukiwaikiliza Koraan na ukasoma Torati katika Agano la Kale utakuta wanazungumza lugha ile ile, wote wanamwamini Mungu mmoja, sasa Mungu mmoja alisema tugombane au tumuabudu…” alieleza na kuhoji.
Wsira alisema nchi imejengwa kuwa ya watu wenye umoja ambao hawagombani kwa makabila, hawabuguani kwa dini na hayo ni mambo nadra katika nchi nyingi barani Afrika.
“Afrika ninayoijua ina matatizo mengi na kwa sababu ya umoja, amani katika nchi yetu tumekuwa nchi ya amani, sisi tuna historia ya zaidi ya miaka 60, katika muda wote huo hamjasikia mambo yanayotokea nchi nyingine yanatokea katika nchi yetu, hamjasikia majeshi yetu yanapindua, hamjasikia watu wanapigana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu tumejenga nchi yenye umoja ambayo ina uhuru wa kila mtu kuabudu, uhuru wa maoni, kila mtu anaweza kutoa maoni, hayo ndio mafanikio tuliyoyapata na sisi mafanikio hayo tuyadumishe.
“Nilitaka kuanzia hapo kuwaambia sisi ni Chama tofauti na vyama vingi ambavyo viko nchini na hiyo ni historia, lakini kazi ya chama chetu inatakiwa kuendelezwa historia hiyo ambayo imeleta amani, umoja na mshikamano katika nchi yetu...
“Nataka kuwaambia nchi yetu bado umoja ni mkubwa sana na nchi yetu bado kuna amani ya kutosha, Rais Kikwete (Dk. Jakaya Kikwete Rais Mstaafu) aliwahi kutuambia zamani nchi haiwezi kupoa kama ugali wa jana, wakati wote ugali wa moto unatoa moshi sasa ukiogopa moshi kula ugali utapata shida, kama unatafuta ule kama kiporo hiyo ni shauri yako lakini ugali unaotoa moshi hauzuii mwenye njaa ashindwe kula maana ule ni moshi sio moto.
Alisema CCM na serikali wanaendeleza juhudi za kujenga umoja na kwamba hali hiyo ndio iliyomfanya Rais Dk. Samia kuendelea kuaminiwa.
== ==
MAELEZO PICHA
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Ndg. Stephen Wasira akizungumza na Wanachama pamoja na viongozi mbalimbali wa CCM Wilaya ya Tunduru, Leo Juni 10, 2025 akiwa Katika Tiara make ya kukagua Uhai wa Chama Mkoa wa Songea.//
No comments:
Post a Comment