Viongozi, Wafanyakazi wa Serikali, Taasisi binafsi, Wafanyabiashara na Wajasiriamali Nchini wameshauriwa kushiriki katika mapokezi na Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, unaotarajiwa kuwasili Visiwani Zanzibar, tarehe 17 mwezi huu.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita, ametoa wito huo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbalo huko Wizarani kwake Migombani Wilaya ya Mjini.
Amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, zinaendelea kuelimisha na kuhamasisha masuala mbalimbali ya kijamii, ikiwemo kuzingatia lishe bora, mapambano dhidi ya Rushwa, VVU/UKIMWI, Matumizi ya Dawa za kulevya na Ugonjwa wa Malaria.
Aidha Mhe. Tabia, kwa niaba ya Waziri mwenzake wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu wa Mhe. Ridhiwan Jakaya Kikwete amewapongeza na kuzishukuru Mamlaka za Mikoa, Wilaya na Halmashauri kwa maandalizi mazuri ya kuupokea na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa, 2025.
Hata hivyo amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluh Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi kutokana na Uongozi bora wa kuwatumikia Wananchi wao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Vijana Shaibu Ibrahim Mohammed amesema kila mwaka, unapokaribia muda wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru Zanzibar, Wizara husika, inatoa taarifa maalum kwa jamii.
Amesema Taarifa hiyo, ni kwa ajili ya kuijuilisha jamii juu ya ujio wa Mwenge na Ratiba yake, kuwakaribisha Wakimbiza Wwenge kitaifa pamoja na kutoa wito kwa Wananchi, Viongozi na Taasisi mbalimbali kushirikiana na wakimbiza Mwenge hao katika Mikoa yote ya Zanzibar.
Mwenge wa Uhuru mwaka huu, unatarajiwa kuwasili katika Kisiwani cha Unguja, tarehe 17-23 Juni 2025, na kuelekea Kisiwani Pemba tarehe 24-27 June, 2025, ambapo Kaulimbiu ya Mwaka huu ni "Jitokeze Kushiriki Uchanguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu ".
No comments:
Post a Comment