Habari za Punde

Waziri Mkuu Amwakilisha Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na Kongamano la Kitaifa la Tiba pamoja na maadhimisho ya miaka 60 ya MAT

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya  (NHIF) mkoa wa Arusha  Isaya Shakif, kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na Kongamano la Kitaifa la Tiba pamoja na maadhimisho ya miaka 60 ya MAT, kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha jijini Arusha, Juni 18, 2025. Mheshimiwa Majaliwa alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kongamano hilo
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Mkurugenzi wa Huduma za Moyo, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)Dkt. Tatizo Waane, kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na Kongamano la Kitaifa la Tiba pamoja na maadhimisho ya miaka 60 ya MAT, kwenye ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha jijini Arusha, Juni 18, 2025. Mheshimiwa Majaliwa alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kongamano hilo. 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na Kongamano la Kitaifa la Tiba pamoja na maadhimisho ya miaka 60 ya MAT, wakati alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mkutano huo uliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha jijini Arusha, Juni 18, 2025.

 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa mabaraza ya kitaaluma, Chama cha Madaktari na  vyama vingine vya kitaaluma kukemea vitendo vilivyo kinyume na maadili ya taaluma na kuchafua taswira ya fani hiyo.

 

Ametoa wito huo leo Jumatano (Juni 18, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na Kongamano la Kitaifa la Tiba pamoja na maadhimisho ya miaka 60 ya MAT, kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha, jijini Arusha.

 

”Wataalamu wote wa afya zingatieni miiko na maadili ya taaluma zenu kwa kutoa huduma bora kwa wananchi. Kila mmoja achukue wajibu wa kuwaonya wale wanaochafua taswira na heshima ya kada hii kwa tabia zisizofaa za uzembe, lugha zisizo na staha, rushwa, wizi wa dawa na vifaa”

 

Ķuhusu jitihada za Serikali za kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeongeza vituo vya kutolea huduma za afya  kutoka vituo 8,549 mwaka 2021 hadi vituo 12,846 sawa na ongezeko la vituo 4,297.

 

“Ongezeko hili la vituo limewezesha asilimia 80 ya wananchi kupata huduma za afya ndani ya umbali wa kilomita tano. Mpango wa serikali ni kufikia asilimia 95 ya wananchi ifikapo mwaka 2030 watakaopata huduma karibu na makazi yao”.

 

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanikisha kutekeleza kampeni maalum ya kufikisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi hadi Hospitali za Halmashauri ambapo jumla ya Madaktari Bingwa 250 walishiriki kutoa huduma katika kambi mbalimbali hapa nchini.

 

Kadhalika, Amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne, Serikali imeongeza MRI kutoka saba hadi kufikia 13, CT Scan zimeongezeka kutoka 12 hadi 45, Ultrasound kutoka 476 hadi 970, Digital X-ray kutoka 147 hadi 491. “Kadhalika ili kufanikisha uchunguzi na ufuatiliaji wa ugonjwa wa saratani, Serikali imenunua PET CT - Scan yenye thamani ya Shilingi Bilioni 18.5”.

 

Ameongeza kuwa, Katika kukabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya kisera ya baadhi ya wadau wa sekta ya afya, Serikali imefanya tathmini ya namna ya kukabiliana na hali hiyo na tayari kiasi cha shilingi bilioni 141.9 kimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa na bidhaa nyingine za afya.

 

Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amepongeza Rais Dkt. Samia kwa kutoa kiasi cha shilingi trilioni 6.7 ambazo kwa kiasi kikubwa zimezifanya Tanzania kuwa kinara katika sekta ya afya miongoni mwa Mataifa mengi “kiasi hiki mageuzi makubwa katika sekta ya afya nchini”

 

 (Mwisho)

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S. L. P. 980,

41193 – DODOMA.

JUMATANO, JUNI 18, 2025.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.