Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na Watanzania wote katika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika yenye kauli mbiu “Haki za Mtoto; Tulipotoka, Tulipo na Tuendako.”
Kupitia kauli mbiu ya mwaka huu, THBUB inaendelea kuhamasisha
jamii kuheshimu na
na kulinda haki za mtoto kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Sheria,
Seraa na Miongozo mbalimbali inayolinda haki za mtoto nchini.
Maadhimisho ya mwaka huu yanalenga kuwaelimisha na
kuwakumbusha wazazi na walezi kwenye jamii pamoja na watoa huduma wote, wajibu
wao katika kutekeleza haki ya 5 za mtoto
zikiwemo Haki ya kuishi kwa mtoto bila ya kukatishwa uhai wake, haki ya
kuendelezwa kielimu, utamaduni na vipaji
vya mtoto, haki ya kulindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote, haki ya kushiriki
kutoa maoni kwenhye masuala yanayomuhusu kulingana na umri wake na haki ya kutobaguliwa kutokana na hali yake.
THBUB inatambua na kuunga mkono juhudi mbalimbali
zinazochukuliwa na Serikali katika kulinda haki za watoto pamoja na kuridhia
Mikataba ya Kikanda na Kimataifa, kutunga Sera na Sheria ya Mtoto ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na ya Zanzibar ambazo zinalinda haki za watoto.
Pamoja na jitihada mbalimbali zilizochukuliwa bado zina zipo
changamoto kadhaa ambazo zinarudisha nyuma juhudi za uapatikanaji wa haki za
watoto.
Changamoto hizo ni pamoja na watoto kubakwa, kulawitiwa,
kuolewa wakiwa na umri mdogo, kuteswa, kufanyishwa kazi ngumu, kukatishwa
masomo, kuuliwa kwa imani za ushirikina, kushirikishwa kwenye ngono, watoto
wenyeulemavu kufichwa n.k hali inayoathiri ukuaji wao.
Hivyo, Tume inatoa mapendekezo yafuatayo.
i. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
iendelee kutoa elimu ya haki za matoto na ukatili wa kijinsia na madhara yake.
ii. Jamii iwafichue watu wote wanashiriki kufanya
ukatili dhidi ya watoto.
iii. Jamii iwafichue wazazi/walezi wote wanaokatisha
masomo watoto kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kuwalazimisha kuolewa.
iv. Serikali iendelee kuchukua hatua kali kwa yeyote
atakayemuajiri mtoto na kumazimisha kufanya kazi ngumu.
v. Wazazi na walezi wahakikishe wanawatunza,
kuwalinda na kuwapatia watoto mahitaji yao ya msingi. Aidha, wahakikishe watoto
wote wanahudhuria shule na hawawatumii kama vitega uchumi vya familia kwa
kuwafanyisha kazi ngumu, zisizofaa na zinazowaathiri.
“Haki
za Mtoto; Tulipotoka, Tulipo na Tuendako”
Imetolewa na:
Mathew
P. M. Mwaimu (Jaji Mstaafu)
MWENYEKITI
TUME
YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
No comments:
Post a Comment