Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zimbabwe zimeazimia kuimarisha ushirikiano wao wa kihistoria kwa kulenga sekta muhimu za maendeleo ikiwemo biashara na uwekezaji,ulinzi, teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT), elimu na mafunzo, utalii, utamaduni na michezo na masuala ya uhamiaji.
Maazimio hayo yamefikiwa leo Julai 25, 2025 kwenye mazungumzo yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Mkutano wa 27 wa Kamati ya Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya Masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama (MCO), kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Prof. Amon Murwira jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, mawaziri hao wameelezea dhamira ya nchi zao kukuza ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Kwa upande wake Waziri Kombo alieleza kuwa Zimbabwe ni mshirika wa muda mrefu wa Tanzania na kwamba kuna fursa nyingi za kimaendeleo ambazo nchi hizi mbili zinaweza kuzitumia kwa pamoja kwa manufaa ya wananchi wake.
“Tanzania na Zimbabwe zina historia ya pamoja katika harakati za ukombozi wa Afrika, na sasa tunapaswa kutumia uhusiano huo kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo unaogusa maisha ya wananchi wetu na vilevile kuhakikisha kizazi kipya kinapewa taarifa muhimu ili waweze kuenzi na kuendeleza mambo mazuri yaliyoanzishwa na waasisi wetu.” alisema Mhe. Balozi Kombo.
Kwa upande wake, Mhe. Prof. Murwira alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya juu, utafiti, na ubunifu kama injini za maendeleo ya uchumi wa kisasa. Alieleza kuwa Zimbabwe ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuanzisha programu za kubadilishana wanafunzi, watafiti na walimu wa vyuo vikuu.
“Ushirikiano wa kielimu utasaidia kuandaa kizazi kipya cha viongozi na wataalam watakaosukuma mbele ajenda za maendeleo ya bara letu,” alisema Prof. Murwira.
Mbali na hayo, viongozi hao wawili wamejadili masuala ya kikanda na kimataifa, ikiwemo hali ya usalama katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), mabadiliko ya tabia nchi na umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya biashara baina ya mataifa hayo mawili rafiki na Afrika kupitia Mpango wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).
Pande zote mbili zimekubaliana kufanya mikutano ya mara kwa mara ya tume ya pamoja ya ushirikiano (JPC) kwa ajili ya kuharakisha na kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa makubaliano na mipango ya pamoja iliyofikiwa.
Mkutano huu ni sehemu ya juhudi za kidiplomasia za Tanzania kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na mataifa jirani na washirika wa kihistoria, sambamba na sera ya sasa ya diplomasia ya uchumi inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
No comments:
Post a Comment