KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fatma Hamad Rajab, ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuziunga mkono timu za michezo ili kuongeza hamasa na kukuza vipaji kwa vijana.
Akizungumza katika uwanja wa Mao Zedong, wakati wa fainali za Kombe la Karume Cup kati ya timu za wanawake na wanaume zilizofanyika usiku wa kuamkia jana alisema wadau na wadhamini wanapaswa kushirikiana na serikali kuendeleza michezo, jambo litakalosaidia kuinua viwango vya ushindani na kuinua uchumi wa taifa.
Aidha alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa uwekezaji katika ujenzi wa viwanja vipya na ukarabati wa miundombinu ya zamani ya michezo, sambamba na ujenzi wa hosteli za mafunzo, akisema hatua hiyo inalenga kuibua na kuendeleza vipaji Kwa vijana.
“Michezo ni ajira, michezo ni fursa. tuwaunge mkono. vijana wetu ili kuhakikisha wanacheza katika mazingira salama na kufanikisha malengo ya ndoto zao,” alisema.
Aliongeza kuwa uwekezaji na msaada kwa vijana katika michezo utasaidia kuibua vipaji vya aina mbalimbali na kuchochea hamasa ya jamii, pamoja na kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi.
Katibu Fatma akitoa shukrani Kwa Familia ya Muasisi na Mkombozi wa Nchi Marehemu Abeid Amani Karume Kwa kushirikiana na Zayadesa kwa kuuufanya mchezo huo wa kikapu kutambulika na Jamii .
Nae Mdhamini wa Mashindano ya Karume Cup, Ahmed Amani Karume, alisema lengo la kuandaa mashindano hayo ni kumkumbuka na kumuenzi Marehemu Mzee wao, ambaye alikuwa akiwajali vijana kwa kuwasaidia na kuwaunga mkono.
Alisisitiza kuwa hali hiyo imewapa nguvu na hamasa ya kuendeleza michezo, hususan kwa kuunga mkono timu za vijana wenye umri chini ya miaka 18.
“Uzuri wa mchezo wa mpira wa kikapu ni kwamba unavutia kwa wanaume na wanawake, jambo ambalo lina umuhimu mkubwa katika jamii,” alisema mdhamini huyo.
Kwa Upande wa Katibu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Zanzibar, Thani Mfaume Lali, alisema shirikisho litachukua hatua za kinidhamu kwa wale wote watakaokuwa na nia ya kuvuruga mchezo huo.
Akizungumza katika mashindano ya Kombe la Karume Cup, Thani alisema safari za kurejesha matumaini zimeanza upya baada ya miaka mitano bila mdhamini, na sasa mashirikiano kati ya mdhamini na wapenzi wa mpira wa kikapu yanaanza kuzaa matunda.
Jumla ya timu 24 za wanaume, wanawake na watu wenye ulemavu zilishiriki katika mashindano hayo. Ambapo kwa wanawake Mafunzo alitwaa ubingwa kwa ushindi wa pointi 53-49 wakati Miembeni ilishinda kwa pointi 58-47 kwa upande wa wanaume.
Shirikisho limezitaka timu zote kuendelea kushirikiana na kuheshimu kanuni, huku likihamasisha amani na utulivu kwa ajili ya kukuza michezo na afya bora kwa jamii, kama nguvu kazi ya taifa.
Imetolewa na Kitengo cha Habari
WHVUM.
No comments:
Post a Comment