MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya usafiri na usafirishaji ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa kituo cha gari za abiria Mndo, wilaya ya magharibi ‘A’ mkoa wa mjini magharibi.
Amesema kituo hicho cha abiria katika eneo hilo kitarahisisha upatikanaji wa huduma mbali mbali kwa wananchi ikiwemo kufika kwa haraka katika maeneo ya utoaji wa huduma kama vile hospitali, sokoni, skulini, sehemu zinazotolewa huduma za fedha na nyenginezo.
Amefahamisha kuwa kituo hicho kitatoa fursa za ajira kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kutokana na kuwepo maduka na mikahawa ambayo kwa pamoja vitachochea shughuli za kibiashara.
Aidha, amesema kituo hicho kitaliwezesha Baraza la Manispaa Magharibi ‘A’ kuongeza ukusanyaji mapato yatakayotumika katika kuimarisha utoaji na upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema katika mwaka wa fedhia 2025/2025 Baraza la Manispaa hiyo limetenga bajeti kwa ajili ya kujenga zaidi ya maduka 25, kituo cha mafuta (sheli), kituo cha kufurahishia watoto na kituo kidogo cha kisasa cha gari za abiria katika eneo la Fuoni Mambosasa.
Alisema ujenzi wa vituo hivyo vitachochea ukuwaji wa uchumi, kuimarisha haiba ya wilaya ya manispaa hiyo na kuongeza vyanzo vipya vya mapato.
Ametoa wito kwa wananchi watakaobahatika kufanya shughuli zao katika kituo hicho kutunza miundombinu iliyopo ili idumu kwa muda mrefu na kuleta tija kwa wananchi na serikali kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Hamza Hassan Juma, amesema kituo hicho ni miongoni mwa miradi iliyolenga kutatua changamoto za wananchi na kutimiza matakwa ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.
Amesema kituo hicho kitataoa faida nyingi chanya kwa wakaazi wa maeneo hayo na jirani ikiweno kupatikana kwa urahisi huduma za usafiri na usafirishaji, ajira na kuongeza mapato.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale ambae ni mgombea wa uwakilishi wa jimbo la Bububu kupitia CCM, Mudrik Ramadhan Soraga, alisema serikali imejikita kuwaondolea wananchi changa kero mbali mbali zinazowakabili ambapo jimbo la Bububu limenufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara, elimu, maji safi na salama, vituo vya usafiri na miradidi mengine ya maendeleo.
Soraga amesema wananchi wa Bububu wanaahidi kumrejesha tena madarakani Rais Dk. Mwinyi wakiamini kuwa mengi mazuri yataendelea kupatikana katika jimbo hilo na Zanzibar kwa ujumla.
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Issa Mahfoudh Haji, alisema ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk Hussein Mwinyi wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2020.
Amesema lengo la kujengwa kituo hicho ni kurahisisha huduma ya usafiri na usafirishaji kwa maeneo ya Kizimbani na vijiji jirani na upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii.
Amefahamisha kuwa ujenzi wa kituo hicho umegharimu zaidi ya shilingi milioni 870 zilizotolewa na Baraza la Manispaa Magharibi ‘A’ ambao umejumuisha barabara, mkahawa, maduka, vyoo na sehemu ya kuegeshea gari.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR )
Tarehe 26.08.2025.
No comments:
Post a Comment