Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa akigonga kengele kuashiria kufungua kwa soko la hisa wakati alipotembelea Ofisi za Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) zilizopo Morocco, jijini Dar es Salaam, Agosti 26, 2025. Kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Situmbeko na Jaji Muu Mstaafu Mohammed Othaman Chande
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipotembelea Ofisi za Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) zilizopo Morocco, jijini Dar es Salaam, Agosti 26, 2025 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amelipongeza Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa kuongezeka kwa thamani ya soko hilo na kufikia shilingi trilioni 21.0 katika kipindi cha kufikia julai 2025.
Amesema kuwa pia soko hilo limeongeza ukuaji wa mauzo ya hisa kwa zaidi ya asilimia 246 pamoja na ongezeko la idadi ya wawekezaji hadi zaidi ya akaunti 683,000 ikiwa ni ishara ya ukuaji imara wa sekta ya mitaji nchini
Amesema hayo leo Jumanne (Agosti 26, 2025) alipotembelea Ofisi za soko hilo zilizopo Morocco, jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kipindi hicho mauzo ya hatifungani yaliyofikia zaidi ya shilingi trilioni 3 pamoja na hatifungani zenye maudhui ya kusaidia mazingira na jamii. “Hiki ni kielelezo cha ubunifu na mchango wa DSE katika kuendeleza uchumi jumuishi na endelevu wa Taifa letu, hii hatuwezi acha ikapita ni lazima tuwapongeze”.
Akizungumza katika mkutano huo, Mheshimiwa Majaliwa ametangaza kununua hisa zenye thamani ya shilingi milioni 100 katika soko la hisa la Dar es Salaam.
“Watanzania wekeni kipaumbele cha kufanya uwekezaji kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa njia ya kidigitali ili kupata fursa ya kuwa sehemu ya kumiliki makampuni na kupata fedha kupitia faida inayotengenezwa na kampuni na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa letu.”
Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Fedha iendelee kushirikiana na DSE katika kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wote ili kuhakikisha fursa zinazotolewa na soko hilo zinanufaisha Watanzania wengi zaidi.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, amesema ili kufanikisha malengo ya dira Taifa ya Maendeleo ya 2050 Serikali imeweka mpango wa kuendeleza bidhaa mpya za kifedha kama vile hati fungani, kuimarisha mifumo ya kidijitali katika soko la DSE ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi wakiwemo Diaspora.
Amesema eneo lingine ni kuendeleza ushirikiano na sekta binafsi na wadau wa kikanda, kuongeza ushiriki wa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuongeza ukuaji wa soko la DSE.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)Charles Shirima amesema ili kuwezesha ushiriki wa wananchi wengi mijini na vijijini katika uwekezaji wa masoko ya mitaji, mamlaka hiyo imehimiza matumizi ya mifumo bunifu katika uuzaji na ununuzi wa dhamana za masoko ya mitaji kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ikiwa ni pamoja na simu za mikononi na intaneti.
Amesema jitihada hizi zimewezesha kuanzishwa kwa mifumo kadhaa ikiwepo ya Sim Invest, Hisa Kiganjani, WekezaWHI na M-Wekeza ambayo inatumika kurahisisha upatikanaji wa huduma za masoko ya mitaji kwa wananchi wengi zaidi mijini na vijijini.
"Kwa mfano asilimia 24.33 ya mauzo ya hisa kwa mwaka 2024, yalipitia katika mfumo wa teknolojia ya habari yakiwa yameongezeka kutoka asilimia 4.84 mwaka 2023."
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Situmbeko amesema tangu kuanzishwa kwake, soko hilo limeendelea kuongezeka thamani ya mauzo ya hisa pamoja na hamasa kwa wawekezaji.
Amesema thamani ya mauzo ya hisa ilifikia shilingi bilioni 369.4 sawa na ongezeko la asilimia 246 ikilinganishwa na kipindi kama hichi mwaka jana.
"Kiasi cha hisa zilizouzwa zilifikia milioni 272 ambalo ni ongezelo la asilimia 108 ikilinganishwa na kipindi kama hichi mwaka jana, hatifungani za Serikali pamoja na makampuni binafsi zilifikia jumia ya mauzo ya zaidi ya shilingi trilioni 3 katika kipindi kama hichi mwaka jana mauzo haya yalifikia shilingi trillioni 1.9"
No comments:
Post a Comment