Habari za Punde

DKT.BITEKO AKIFUNGA KIKAO KAZI CHA WENYEVITI WA BODI NA WAKUU WA TAASISI ARUSHA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akifunga Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CE.Os Forum 2025) kilichofanyika jijini Arusha katika Ukumbi wa AICC
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akimkabidhi Cheti Mwenyekiti wa Bodi ya Hifadhi ya Ngorongoro, Jenerali Venance Mabeyo wakati wa ufungaji wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs Forum 2025) kilichofanyika Agosti 26, 2025 katika Ukumbi wa AICC Jijini Arusha. Cheti hicho kimekabidhiwa kwa kuwa NCAA imekuwa sehemu ya wadhamini wa kikao hicho.

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza Wenyeviti na Wakuu wa  Taasisi za Umma nchini kusimamia utekelezaji wa maazimio ya kimkakati yanayofikiwa katika vikao kazi wanavyofanya kwa kutambua kuwa wamebeba dhamana ya kuboresha maisha ya
Watanzania kupitia mtaji wa shilingi Trilioni 86 ambao Serikali imewekeza kwenye Taasisi na mashirika yake..

Dkt. Biteko ameyasema hayo tarehe 26 Agosti 2025 jijini Arusha wakati akifunga kikao kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (CEOs FORUM 2025).

“Watanzania wanawategemea ninyi kuwabadilishia maisha, kama tunazungumza kuhusu umaskini wa watu, Serikali inapaswa kuwa kiongozi wa kuwaondolea watu umaskini wao,
hivyo hamna budi kutambua  kuwa mnalo deni la kuboresha hali zetu na maisha yetu.” Amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko amewahakikishia Watendaji hao kuwa Serikali katika ngazi zote inatambua mchango wa taasisi na mashirika katika ukuaji wa uchumi na pia inatambua mchango wa vikao
kazi vya watendaji hao ambavyo vimepelekea mashirika kuongeza mchango wake katika mfuko mkuu wa Taifa.

" Vikao kazi hivi mnavyofanya vimeonesha mchango wake katika uchumi, mfano katika kikao kazi cha mwaka 2024 mliazimia mashirika ya umma yaboreshe utendaji na  kuongeza uchangiaji katika mfuko mkuu wa Serikali na  matokeo yameonekana mfano Shirika la Maendeleo ya Petroli
( TPDC) liliongeza uchangiaji wake kwa asilimia 100, shirika hili liliongeza uchangiaji wake kutoka shilingi bilioni 5.5 kwa mwaka 2023/2024 hadi shilingi bilioni 11.1 mwaka 2024/2025." Amesema Dkt.Biteko

Ameongeza kuwa, uchagiaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) umeongezeka kwa  asilimia 363 katika mfuko mkuu wa Serikali ambapo NHC ilichangia shilingi bilioni 1.2 mwaka 2023/ 24 na mwaka 2024/2025 ilichangia shilingi bilioni 5.5.

Dkt. Biteko amewaeleza Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi kuwa “Rais Samia pamoja na kuthamini mchango wenu kwa Serikali anatarajia mengi kutoka kwenu na Watanzania wana matarajio makubwa hasa wakati tukielekea kwenye  utekelezaji wa Dira 2050, endeleeni  kuongeza mchango wenu kwenye  ukuaji wa uchumi, mjitegemee na muwe mfano wa
taasisi binafsi."

Katika.hatua nyingine, Dkt. Biteko ametaka viongozi hao kufanyia kazi agizo lililotolewa na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango la  kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato.

Pia amempongeza Msajili wa Hazina kwa kuwa na maono ya kuratibu kikao kazi hicho ili kujadili masuala yatakayosukuma mbele utendaji wa taasisi.

Katika hafla hiyo, Dkt. Biteko hakuacha kukumbusha kuhusu ushiriki wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambapo amesema uchaguzi huo uwe ni ajenda ya watu wote wakiwemo Wenyeviti  wa Bodi na Wakuu wa Taasisi hivyo waone kuwa wana wajibu wa kuwasisitiza watu kwenye taasisi zao kujitokeza kusikiliza wagombea na baadaye kupiga kura  kwa amani kwani kukiwa na amani mashirika hayo pia
yatafanya vizuri zaidi.

Naibu Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo kwa upande wake, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan   kwa dira na muongozo katika kuendeleza mashirika ya umma ili yaweze kuwa na tija
nchini.

Amesema katika siku tatu za kikao kazi washiriki wamejifunza na kubadilishana uzoefu kupitia watoa mada wa ndani na nje ya nchi waliobobea.

Amesema Wizara ya Mipango na Uwekezaji itahakikisha maazimio ya  kikao kazi hicho yanatekelezwa ipasavyo, pia Wizara itasimamia mageuzi ya kuhakikisha mashirika  ya umma yanachangia ukuaji wa pato la taifa hadi kufikia Dola  za Marekani trilioni 1  ifikapo 2050 ambapo  kwa sasa pato la taifa ni dola za Marekani bilioni 85.

Kwa upande wake Salim Kali, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema wilaya 6 za Mkoa wa Arusha zimefikiwa na umeme hadi ngazi ya vijiji, pia  miradi ya maji imefanyika pamoja na  miundombinu ya Barabara ambayo imewezesha maisha bora kwa watu wa aina zote wakiwemo watalii.

Awali, Msajili wa Hazina,  Nehemia Mchechu alisema kuwa katika kikao kazi hicho kampuni zaidi 300 zimeshiriki huku washiriki wakiwa ni zaidi ya 650.

Alisema kikao kilikuwa na  majadiliano mbalimbali ya kina yanayolenga kusukuma mbele uchumi wa nchi na kusimamia uwekezaji wa Serikali  kwa taasisi za umma wa zaidi ya shilingi trilioni 86.

Mkutano huo wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma uliongozwa na kaulimbiu ya  "Ushirikiano Endelevu wa  Kibiashara katika Mazingira Shindani Kimataifa- Nafasi ya Mashirika ya Umma."

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.