WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewaagiza waendeshaji wa awamu ya pili ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT-2) kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha maeneo yaliyobaki yatakayowezesha mradi huo kuanza kutoa huduma ndani ya muda mfupi.
Amesema hayo leo Jumatano (Agosti 13, 2025) wakati alipokagua mabasi mapya kwa ajili ya awamu ya pili ya mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT-2) pamoja na miundombinu ikiwemo kituo kikuu cha mabasi hayo cha Mbagala Rangi tatu na kituo cha gerezani, jijini Dar es Salaam. Pia alitembelea ujenzi wa kituo maalum cha kujazia gesi kwa ajili ya mabasi hayo, kinachojengwa katika kituo cha Mbagala Rangi Tatu.
“Tunataka mradi huu uanze kutoa huduma kwa Watanzania hasa wakazi wa Dar es salaam, mradi huu utaongeza ufanisi wa usafiri wa umma katika jijini la Dar es Salaam na kutoa huduma ya kisasa, salama na ya haraka kwa wananchi.”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya utoaji huduma ya Usafiri ya Mofat Mohammad Kassim kuhakikisha anakamilisha haraka taratibu za utoaji wa mabasi 99 yaliyopo bandarini ili kuwezesha huduma hiyo kuanza kwa wakati.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inataka kuona katika awamu ya pili ya mradi wa BRT, tiketi za usafiri kupitia mabasi hayo zinakuwa za kielektoniki badala ya tiketi za karatasi kama ilivyokuwa awali. “Tukifanya hivi itatusaidia kumonitor kiasi cha fedha kinachokusanywa.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa za ajira zitakazotokana na mradi huo ikiwemo udereva.
“Nendeni mkasome masuala ya udereva kupitia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), mradi huu utahitaji idadi kubwa ya madereva wenye ujuzi”.
Akizungumza baada ya kukagua kituo cha kujazia gesi kwenye mabasi hayo kilichopo kwenye kituo kikuu cha Mbagala Rangi Tatu, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza kampuni ya Lake Oil inayotekeleza mradi huo kuhakikisha wanakamilisha usimikaji wa mitambo ili waanze kutoa huduma.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliambana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) William Lukuvi, Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Zainab Katimba, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi pamoja na watendaji wengine wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na Chuo cha Taifa cha usafirishaji (NIT).
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO , AGOSTI 13, 2025
No comments:
Post a Comment