Wizara ya Afya kupitia idara ya ufundi na miundombinu ya Afya imefanya ziara ya kukagua vituo vya Afya vinavyotarajiwa kupokea wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika hospitali ya Mnazimmoja kwa lengo la kupisha ujenzi wa hospitali hiyo unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Akizungumza baada ya kukamilisha ziara hiyo iliohusisha nyumba za madaktari zilizopo katika Hospitali ya Mwera Pongwe pamoja na Kitogani Mkurugenzi ufundi na miundombinu ya Afya Qs.Amina Mohamed Habibu.
Amesema lengo la ziara hiyo ni kuhakikisha wanatengeneza ukaribu wa upatikanaji wa huduma za kujifungua kwa mama wajawazito waliokuwa wakitumia Hospitali ya Mnazi mmoja kwa kutumia Vituo vya Afya vilivyopo Mjini na kuwapunguzia usumbufu wa kuzifuata huduma hizo katika hospitali za Wilaya.
Amewaagiza wakandarasi wanaoshughulikia vituo hivyo kuzingatia muda uliowekwa ili kuona vinapokea wagonjwa hao na kutoa huduma za matibabu katika muda uliopangwa.
Aidha amewaasa wananchi kuendelea kuiamini serikali kupitia Wizara ya Afya kwani itahakikisha wagonjwa watakaohamishiwa katika vituo hivyo watapatiwa huduma sawa na bora kama walizokuwa wakizipata katika hospitali ya Mnazi mmoja.
Akigusia Nyumba za Madaktari Qs.Amina amesema hadi kufikia sasa ujenzi wa nyumba hizo unaridhisha licha ya kuwepo kwa mapungufu madogo madogo ambayo amewaagiza wakandarasi kuyakamilisha kabla ya kuzikabidhi kwa Serikali.
Amesema hadi sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya imejenga Nyumba za madaktari zenye uwezo wa kuhudumia familia kumi na sita kwa awamu hii ya kwanza Unguja na Pemba zenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma za Afya kwa wagonjwa wanaofuata huduma kwenye hospitali hizo.
Kwa upande wake Mshauri elekezi kutoka kampuni ya Mecon Arc Consult Hanifa salum Abdallah akaahidi kuzifanyia kazi baadhi ya kasoro zilizoonekana kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanakabidhi nyumba hizo kwa serikali zikiwa zimekamilika.
Ziara hiyo imehusisha Kituo cha afya cha Imani, Nyumba za madaktari Mwera Pongwe pamoja na Kitogani.
No comments:
Post a Comment