Imeandikwa na Faraja Mgwabati – Habari Leo
Mara ya kwanza nilipofika visiwa vya Unguja na Pemba, mwaka jana, nilipata shida kidogo kuzoea namna ambavyo utamaduni wa wenyeji wa huko ulivyo. Kila jambo linafanywa kwa polepole kama vile watu hawana haraka ya kufanya mambo mengine. Baada ya kukaa wiki mbili nilianza kuzoea na mimi nikawa nafanya kama wao.
Tofauti na mara ya kwanza, safari hii nimeingia Unguja nikiwa mwenyeji na ninayejua mazingira ya visiwa hivi, kwa bahati mbaya wenzangu niliokwenda nao inaonekana hawajauzoea utamaduni huo. Jumapili iliyopita tulikuwa katika safari ya kwenda Unguja kuhudhuria mkutano wa Uwekezaji ambao ulifanyika kwenye moja ya fukwe maarufu za mjini hapo.
Tulipokaribia kufika, tulikubaliana kuwa kitu cha kwanza baada ya kufika itakuwa ni kutafuta hoteli halafu chakula, kwani tulikuwa na njaa muda huo, ingawa ulikuwa ni mwendo wa saa mbili kutoka Dar es Salaam. Baada ya kushuka tulichukua teksi hadi hotelini na tukataka kumlipa dereva wa teksi aondoke kwa kuwa tulikuwa tumeshapata vyumba.
Lakini cha kushangaza dereva alisema, ‘Nendeni tu lipieni vyumba, wekeni vitu vyenu mimi mtanikuta nawasubiri.” Tukaingia mapokezi hotelini hapo na kulipia. Mimi nikamwambia mhudumu naomba risiti ya malipo, akasema nitakuandikia tu usijali we endelea utaikuta. Sikushangaa sana kwani niliwahi kukaa hapo mwaka jana.
Hatimaye tukatoka nje tukaonana na dereva wetu, tukamwuliza sehemu gani tunaweza kupata chakula kizuri? Akasema twendeni, akatupeleka sehemu inaitwa CCM ambako mgahawa mpya umefunguliwa. Wenzangu wakamwuliza tukulipe kiasi gani? Akajibu, “Nyie kuleni tu mie nawangoja hapa nje, mie na nyie hatudhuriani ati, hatuwezi gombana tutakubaliana tu!”
Tukaingia ndani bwana, tukakuta kaunta watu wengi wanaagiza na kuchukua chakula huku wengi wao wakichukua kwa ajili ya kwenda kula nyumbani, hali ambayo ilinifanya nimuulize mwenyeji wa huko baadaye kulikoni watu wanabeba ‘takeaway’ nne hadi tano. Akaniambia kuwa wenyeji wa mji huo hawapendi mambo ya kupika, hasa mchana wengi wanakula hotelini na wengine ndo kama vile wanabeba kulingana na familia walizonazo nyumbani kwao.
Wakati tukisubiri kupata huduma, mmoja wa jamaa zangu niliokuwa nao inawezekana alikuwa na njaa au alikuwa amezoea staili ya bara ya kuagiza vitu dukani au hotelini kwani alitaja chakula anachotaka, pilau, zaidi ya mara 15 mhudumu alikuwa anazungumza tu na wateja wengine. Siyo kwamba alikuwa hamsikii, la hasha, ni wazi kwamba alikuwa akimsikia kwani alikuwa karibu yake kabisa lakini akawa anahudumia wanaotaka ‘takeaway’ kwanza na pengine wale anaowajua.
Jamaa yangu alikuwa anaendelea kusisitiza nipe pilau huku akimwonyesha noti ya 10,000, lakini yule mhudumu alikuwa anaendelea kupiga stori na wengine, ikabidi mimi nimbonyeze rafiki yangu na kumwambia tulia kwanza. Baada ya muda kidogo akachukua fedha yake na akatuhudumia. Pilau lilikuwa tamu sana, au inawezekana tuliliona tamu kwa sababu ya njaa zetu.
Tukatoka nje na kumkuta dereva wetu akiwa amejipumzisha kwenye gari akiwa hana hofu yoyote kama ilivyo kwa madereva wa teksi wa Dar es Salaam ambao akikusubiri kidogo anakutoza gharama ya kusubiri, au ukimwambia akusubiri anaona anachelewa wateja wengine. Akaturudisha mpaka hotelini na akatuuliza hamwendi kwingine tena? Tukamwambia hapana, twapumzika tukikuhitaji tutakupigia simu. Kazi iliyobaki ilikuwa ni kupatana bei sasa, tulikuwa tukihofu kwamba atatutajia bei kubwa lakini haikuwa hivyo pamoja na kutusubiri kote.
Sitasema alitutoza kiasi gani lakini tukamwomba atupunguzie 1,000 akakubali. Tulipoingia hotelini nilimkuta mhudumu mwingine ambaye nilimweleza kuwa nilishalipia chumba nahitaji risiti. Naye alinijibu kama yule wa mwanzo, ‘usiwe na wasiwasi nitakuandikia,’ alisema hivyo wakati hakuwa na kazi yoyote pale kaunta.
Katika tukio jingine, mwandishi mwenzangu alikutana na kituko kingine wakati akitoka katika eneo la Kwamchina akielekea Darajani, ambapo alipatwa na butwaa pale alipoona dereva wa daladala walilokuwa wamepanda akisimama ghafla na kuanza kupiga soga na mtembea kwa miguu bila wasiwasi.
Mwenda kwa miguu huyo ambaye inaelekea alikuwa ni ndugu wa dereva, alisimamisha gari na wakaanza kuzungumza mambo yao ya kifamilia takribani dakika tano huku abiria wakiwa kimya wala hawana wasiwasi. “Baada ya kuona muda unazidi kwenda nikawageukia abiria wenzangu labda tujaribu kumkemea dereva, lakini nikaona wote wametulia tu na hakuna anayelalamika, nilishangaa sana,” anasema mwandishi huyo wa gazeti moja la Dar es Salaam.
Tukio jingine ni pale alipokwenda dukani kununua betri, akamwuliza muuzaji una Duracell? Muuzaji akajibu sina, Mwandishi akamwuliza una betri aina nyingine yenye nguvu kama Duracell? Muuzaji akasema sina. Lakini katika kupitisha macho mwandishi akaona betri aina ya Energizer akamwambia muuzaji mbona Energizer naziona? Yule muuzaji akashituka kwa kusema, “Alaa kumbe na hizo watumia?”
Hayo ndiyo mambo ya Unguja lakini kwa ujumla watu wa visiwa hivyo ni wakarimu na wanaopenda wageni, ingawa wapo wanaosema ukarimu wao upo kwenye mambo yote, lakini siyo kwenye chakula. “Hawa jamaa Wazanzibari wanaweza kukupa hata gari lao ukatumia muda wote ukiwa Unguja lakini hata siku moja hawawezi kukukaribisha chakula kwao,” alisema kijana mmoja wa bara lakini amekaa muda mrefu Unguja.
Taarifa ningine zinasema watu wa visiwa hivi hawapendi kupika majumbani mwao ndiyo maana ikifika wakati wa chakula cha mchana utakuta msururu mirefu kwenye migahawa na hoteli wakinunua vyakula kwa ajili ya kula nyumbani. Mpaka naondoka Unguja yule ndugu yangu wa mapokezi hotelini alikuwa hajaniandikia risiti yangu, na mimi nikasahau hivyo nikaondoka bila risiti, hiyo yote ni kwa sababu ya ‘Mambo polepole’.
TANAPA YATUNUKIWA TUZO YA JUU ULAYA KWA MARA YA SITA MFULULIZO
-
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limetunukiwa tuzo ya hadhi ya juu kwa
mara ya sita mfululizo iitwayo European Quality Choice Diamond ya mwaka
2025 k...
1 hour ago
No comments:
Post a Comment