BARAZA la Manispaa Zanzibar limeruhusu kwa muda uendeshaji wa biashara katika eneo la mbele la soko kuu la Darajani, Zanzibar hadi mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa soko la Darajani, Fadhili Khatibu Shaabani amesema hatua hiyo inalengo la kuwarahisishia wananchi kununua bidhaa bila usumbufu.
Alisema kawaida eneo la mbele la soko hilo haliruhusiwi kufanya biashara kwa sababu ya kulinda mandhari ya soko hilo la kihistoria.
" Soko la Darajani ni la kihistoria na linapaswa mandhari yake kuwa nzuri, itunzwe ili iwe kivutio kwa wageni wanaofika Zanzibar," Alisema Fadhili
Hata hivyo, alisema shughuli za kibiashara katika eneo hilo zitasitishwa mara tu baada ya kumalizika kwa ramadhani.
Fadhili alisema pamoja na kutolewa ruhusa hiyo, wafanya biashara watakaopaswa kulitumia eneo hilo ni wale waliopatiwa vibali maalum na Baraza.
Aidha, Baraza limewataka wafanya biashara wa soko hilo kushirikiana na Baraza la Manispaa ili kuona kwamba soko linakuwa safi muda wote.
Kuhusu wafanya biashara wanaofanya biashara sehemu ambazo hazikuruhusiwa alisema Baraza lake litaendelea kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika mahakama ya Baraza hilo hapo malindi.
No comments:
Post a Comment