Habari za Punde

BALOZI AMINA SALUM ALI AIUNGA MKONO SERIKALI KUSUKUMA MAENDELEO YA AKINAMAMA

Na Rajab Mkasaba

MWAKILISHI wa Kudumu wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa, Balozi Amina Salum Ali, ameunga mkono lengo la Serikali ya awamu ya saba nchini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein la kuanzisha Benki ya wanawake hapa Zanzibar kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo yao kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Balozi Amina aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Ikulu, Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Amina alieleza kuwa tayari yeye mwenyewe amechukua hatua za makusudi katika kuhakikisha jambo hilo muhimu la maendeleo ya wanawake linafanikiwa kwa kupitia afisi yake iliyopo Washington, Marekani.

Alieleza matumaini yake kuwa afisi yake itatoa mashirikiano makubwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein katika kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Balozi Amina alieleza kuwa wanawake wanaweza kupata mafanikio makubwa kimaendeleo ambapo Benki hiyo inaweza kuwa chachu ya maendeleo katika sekta zote muhimu.

Aidha, Balozi Amina alieleza lengo lake la kutoa mashirikiano katika mchakato wa uwanzishwaji wa Chuo Kikuu cha wanawake hapa Zanzibar.

Balozi Amina alieleza kuwa kuna haja kwa wanawake kuwekewa mazingira ya kuwawezesha kuendelea na masomo kwa kiwango cha Chuo Kikuu.

Sambamba na hayo, Balozi Amina alieleza hamu ya wawekezaji na wafanyabiashara wa Marekani hasa wale wenye asili ya Afrika ya kutaka kuja kuekeza na kufanya biasahara hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa wawekezaji hao wameonesha nia ya kuekeza hapa Zanzibar hasa katika sekta ya Utalii.
Wakati huo huo, Balozi Amina alichukua nafasi ya kumpongeza Dk. Shein kwa mara nyengine tena kufuatia ushindi alioupata katika uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni na hatimae kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar awamu ya saba chini ya serikali ya mfumo wa Umoja wa Kitaifa.

Nae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi kwa Balozi Amina kwa ujio wake huo wa mazungumzo pamoja na kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar.

Dk. Shein alimueleza Balozi Amina kuwa wazo la kuanzishwa kwa Benki ya wanawake hapa Zanzibar liko kwenye serikali anayoiongoza.Alisema kuwa serikali anayoiongoza itahakikisha kuwa inalisimamia vyema suala hilo kwa lengo la kuwainua wanawake kimaendeleo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha wanawake ni wazo zuri sana na litasaidia katika kuimarisha sekta ya elimu hasa kwa upande wa wanawake. Alisema kuwa taratibu za makusudi zitachukuliwa na serikali yake anayoiongoza ili kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa kwa mashirikiano ya pamoja.

Akieleza juu ya mafanikio ya uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni, Dk Shein alieleza kuwa uchaguzi huo ulikuwa ni wa huru na haki na ndio maana umefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa anamatumaini makubwa kuwa amani na utulivu iliyopo nchini itaendelea kuendelezwa na kudumishwa zaidi kwa manufaa ya Wazanzibari wote chini ya serikali ya Umoja wa Kitaifa

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.