Habari za Punde

WANANCHI WAOMBWA KUSAJILI RASILIMALI ZAO KUZIPATIA UHALALI.

Maryam Talib Pemba.

MPANGO wa Kupunguza umasikini nchini Tanzania (MKURABITA) umewashauri wananchi nchini Tanzania kusajili mashamba na biashara zao ili kuzipatia uhalali na kuondosha umasikini.

Kufanya hivyo Kumetajwa kuwa na njia ya kupata uhalali wa umilikaji wa mali hizo utakaomsaidia kuhalalisha umiliki wa mali yake na kuwa endelevu.

Hayo yameelezwa na Afisa Mtambuzi wa ardhi Pemba, Mohamed Salim Abdalla alipokuwa akizungumza na gazeti hili afisini kwake Machomane.

Alieleza kuwa lengo la mradi wa MKURABITA ni kuzisajili rasilimali za wanyonge ili ziweze kutambulika na kupatiwa nyaraka ambazo zitawasaidia katika kubinafsisha rasilimali zao.

Afisa huyo alisema utekelezaji wa mpango huo umeweza kuwasaidia wananchi wa shehiya ya kiungoni Kisiwani Pemba kwa kujua mipaka yao ya mashamba ambayo matatizo yote hayo yaliweza kutatuliwa bila ya watu kufikishana kwenye vyombo vya sheria (mahakamani).

Sambamba na hayo, alisema awamu ya kwanza ya zoezi hilo imemalizika na wananchi waliupokea vyema mradi huo na wameahidi kufanya kila liwezekanalo ili kuweza kusajili mashamba yao pamoja na ardhi ili waweze kuepuka migogoro hapo baadae.

Katika mradi huo, mafanikio mengi yamepatikana ikiwa ni pamoja na vijana wapatao 14 kupata ajira katika shehia ya Kiungoni.

“Nataka wananchi wajitolee kwa moyo mmoja kusajili mashamba na ardhi zao kwani kazi hii inafanywa bure bila ya mwananchi yeyote kutakiwa kuchangia chochote hivyo ni vyema mtu kusajili mapema, na wala mpango huu" Alisisitiza kwamba mpango huo haumaanishi kwamba serkikali inakusudia kuwapora wananchi mali zao kama baadhi ya watu walivyoanza kuupokea.

Mradi huo wa awamu ya pili unatarajiwa kuhusisha shehia ya Pembeni wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.