Habari za Punde

WADAU WAMEOMBWA KUISAIDIA TIMU YA ZANZIBAR HEROES ILI KUWEZA KUFANYA VIZURI MICHUANO YA CHALENJI

Na Aboud Mahmoud


WADAU wa soka visiwani Zanzibar wameombwa kuisaidia timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' kwa hali na mali ili kufanikisha timu hiyo inarudi na ubingwa katika michuano ya Chalenji.

Hayo yamesemwa na wapenzi wa soka visiwani humu wakati walipokutana na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti na kusema kwamba ni njia muafaka kuisaidia timu hiyo ili iweze kufikia nafasi nzuri na hatimae kuukwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Wapenzi hao wa soka walisema kuwa tangu mwaka 1995 timu ya Taifa ya Zanzibar ilipochukuwa ubingwa huo ikiwa chini ya mwalimu Hafidh Badru hadi leo timu hiyo haijapata tena nafasi hiyo.

Hivyo walieleza ni bora kwa Serikali,wafanyabiashara na wadau wa soka kuisaidia timu hiyo ili iweze kufikia kiwango kizuri na kuitangaza vyema nchi kupitia mchezo huo.

"Nikiwa mpenzi wa soka na mwenye uchungu wa nchi yangu, naiomba Serikali pamoja na wafanyabiashara wa makampuni tofauti, kuisaidia timu yetu ya taifa ili ifanye vizuri katika mashindano ya Chalenji,"alisema Juma Wadi.

Wadau hao walisema kuwa mbali na Chama cha Soka Zanzibar kufanikisha na kumleta kocha mkuu wa timu hiyo kutoka nchini Uingereza, lakini kuna mambo muhimu zaidi yanahitajika kufanyiwa wachezaji hao ili waweze kuongeza kiwango chao cha soka.

"Tunaipongeza ZFA pamoja na kampuni ya Future Century ya jijini Dar es Salaam kuona umuhimu wa kutuletea kocha huyu ambae ataweza kuisaidia timu yetu iweze kufika mbali, lakini kuna mahitaji mengine muhimu yanahitajika kupatiwa wachezaji ili waweze kuongeza kiwango chao,"alisema Jaffar Bai.

Michuano ya Chalenji inatarajiwa kuanza kutimu vumbi Novemba 27 mwaka huu katika viwanja mbali mbali vya Tanzania Bara ambapo Zanzibar imepangwa kundi moja na timu za Rwanda, Sudan na Ivory Coast.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.