BARAZA la Ushauri la wazee wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, limempongeza kwa dhati rais mpya wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein.
Taarifa iliyotolewa na Baraza hilo na kusainiwa na Mwenyekiti wake Mzee Makame Mzee, ilieleza pongezi hizo walizozitoa kwa Dk. Shein ni kwa kuchaguliwa na wananchi kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Wazee hao walieleza kuwa kuchaguliwa kwa Dk. Shein kunatokana uamuzi wa Wazanzibari sambamba na kuwa na imani naye ya kuiongoza Zanzibar.
Aidha washauri hao wa CCM, walieleza kuwa Dk. Shein amethibitika kuwa na uwezo na nia ya kuijenga nchi kwa ujasiri, ukakamavu, uvumilivu na uelewa wa siasa huku wananchi wakiwa na matumaini naye.
"Sisi wazee wa Chama cha Mapinduzi tupo tayari kushirikiana na wewe bega kwa bega wakati wowote pahala popote tutakapohitajika kwa ushauri wa maendeleo ya nchi yetu", ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha wazee hao walimtakia mafanikio mema, afya njema na kila la kheri Rais Shein katika kuiongoza serikali mpya ya Umoja wa Kitaifa.
No comments:
Post a Comment