Na Abdulla Ali
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili Rais, Mohammed Aboud Mohammed, amesema kuwa Zanzibar itaanzisha Shirika lake ambalo litakuwa na jukumu la kupima ubora wa viwango na bidhaa zinazoingizwa nchini.
Waziri Aboud alieleza hayo jana Ofisini kwake Vuga mjini hapa alipokuwa akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Samia Suluhu Hassan aliyefika ofisini hapo kumtembelea.
Waziri Aboud alisema kuanzishwa kwa Shirika hilo visiwani hapa itakuwa ndio dawa kupambana na wanaoleta bidhaa feki au kuzalisha bidhaa zilizo chini ya viwango.
Waziri huyo alisema kumekuwepo na wimbi kubwa la uingizwaji bidhaa feki na zile zisizo na ubora hali inayosababisha hasara kwa wananchi na watumiaji wa bidhaa hizo.
“Zanzibar ina nia ya kuanzisha shirika la viwango kwa lengo la kupambana na wanaoleta bidhaa feki au kuzalisha bidhaa zilizo chini ya viwango”, alisema Waziri Aboud.
Aidha waziri huyo, aliwaomba viongozi wa taasisi mbali mbali na watendaji kufikiria vyema kauli zao wanapoisema Zanzibar kwani kauli bidhaa feki au za chini ya viwango zinaweza kuijengea chuki nchi.
Alisema mbali ya hali hiyo kauli kama hizo zisizoingatia busara zinaweza kuathiri kibiashara na utalii sekta ambazo zimekuwa muhimili mkuu wa kiuchumi.
Naye Waziri wa Samia akizungumza katika mkutano huo, alisema kero za Muungano zitapatiwa ufumbuzi kupitia vikao vya pamoja.
Alisema kero hizo kwa kiasi kikubwa zimepatiwa ufumbuzi chini ya Uenyekiti wa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye hivi sasa ni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein.
“Kulikuwa na kero nyingi zilizokuwa zikileta usumbufu kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano, zikiwemo za Sheria ya haki za binaadamu, bahari Kuu, wafanyabiasha wa Visiwani na kodi za watendaji wa Muuungano Zanzibar, lakini asilimia kubwa ya kero hizo zimepatiwa ufumbuzi”, alisema Waziri Samia.
Aidha alisema bado changamoto kwenye eneo la Muungano zipo na kueleza kuwa zinazungumzika ili kuweka hali nzuri ya kustawisha Muungano huo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Khalid Salum Mohammed alisema tatizo kubwa katika utekelezaji wa baadhi ya miradi liko kwa watendaji na sio viongozi wakuu.
Alisema watendaji wenye kugawa miradi hiyo wamekuwa wakisababisha Zanzibar kupata miradi michache ile yenye sura ya kimuungano
No comments:
Post a Comment