Habari za Punde

DK SHEIN AENDELEA NA ZIARA YA KUWASHUKURU WANACCM MKOA WA KASKAZINI UNGUJA

Na Rajab Mkasaba

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewasisitiza viongozi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja kuendeleza umoja na mashirikiano wao katika kukitumikia Chama Cha Mapinduzi ili kiendelee kuongoza na kuwaletea maendeleo wananchi.

Aidha, Dk. Shein aliwapongeza viongozi hao wa CCM wa Mkoa huo kwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi Mkuu ulioendeshwa kwa haki, amani na utulivu mkubwa ambapo umedhihirisha kupevuka kwa demokrasia nchini na kuipa heshima na sifa kubwa Zanzibar Kitaifa na Kimataifa.

Dk. Shein ambaye katika ziara hiyo alifuatana na mkewe Mama Mwanamwema Shein, aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na Viongozi wa CCM, wa Mkoa wa Kasakazini Unguja katika mikutano ya Wilaya zote mbili za Kaskazini A na B. Aidha, mikutano hiyo ilijumuisha viongozi katika ngazi za Majimbo, Wadi, Matawi pamoja na Jumuiya za Chama.

Ikiwa leo ni siku yake ya pili ya ziara katika Wilaya zote kumi za Zanzibar ambapo Dk. Shein alieleza umuhimu ya mashirikiano katika kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi.

Dk. Shein alieleza kuwa wananchi wamekuwa na matumaini makubwa na Serikali yao ya Mapinduzi Zanzibar iliyo katika mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Aidha, Dk. Shein aliwapongeza viongozi hao kwa kushiriki kikamilifu na kwa wingi katika mikutano hiyo.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana hapa Zanzibar kwa kufanya uchaguzi ulio huru, haki na wenye amani na utulivu ambapo nchi nyingi duniani imepongeza na kutoa sifa kubwa kutokana na kuendesha uchaguzi huo.

Katika maelezo yake, Dk Shein alisema kuwa kazi kubwa iliyopo hivi sasa ni kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi kwa vitendo sanjari na kuzitekeleza ahadi alizoahidi kwa wananchi wakati wa Kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.

Rais Shein aliupongeza uongozi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa umahiri na uongozi bora wa kukiogoza Chama Cha Mapinduzi katika Mkoa huo na kusisitiza haja ya viongozi kuendelea kutimiza wajibu wao ipasavyo.

Katika mazungumzo yake Dk. Shein alieleza kuwa mafanikio makubwa yameweza kupatikana katika kuyalinda, kuyaendeleza na kuyadumisha Mapinduzi ya Januari 12, 1964.“Tutaendelea kulinda Mapinduzi yetu na Katiba yetu”,alisema Dk. Shein.

Nae Mama Mwanamwema Shein aliwapongeza viongozi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kuendelea kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi na kukipa ushindi chama hichoi pamoja na kumpa ushindi Dk Ali Mohamed Shein.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Saleh Ramadhan Ferouz kwa niaba ya wanaCCM wote alimpongeza Dk. Shein kwa kufanya kampeni za kistaarabu na kuonesha umahiri mkubwa kama alivyoahidi mwenyewe na kupelekea uchaguzi mkuu kuwa wa huru na wa haki.

Nao viongozi wa Mkoa huo walimpongeza Dk. Shein kwa ushindi alioupata katika uchaguzi mkuu uliopita na kueleza furaha zao kutokana na kutambua uwezo mkubwa wa Dk. Shein katika uongozi.

Walieleza kuwa kuchaguliwa kwa Dk. Shein ndio chaguo sahihi kutokana na uwezo wake huo wa uongozi na umahiri alionao katika medani za siasa na umakini katika kusimamia na kufuatilia mambo.

Aidha, viongozi wao wameahidi kuendelea kushirikiana kwa pamoja na kushirikiana nae Dk. Shein katika kukiendeleza na kukiimarisha Chama Cham Mapinduz ili kiendelee kuwaletea maendeleo wananchi.

Dk. Shein kesho anatarajiwa kuendelea na ziara yake hiyo kwa kukutana na viongozi wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi kwa lengo la kuwashukuru na kuwapongeza viongozi hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.