Habari za Punde

DK SHEIN ATOA SALAMU ZA MWAKA MPYA LEO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK Ali Mohamed Shein akitoa salamu za mwaka mpya wa 2011 kwa wananchi wa Zanzibar leo Ikulu.

Picha na Ramadhan Othman.

RISALA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHE DK. ALI MOHAMED SHEIN, KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2011 A.D., 1432 A.H. – DISEMBA 31, 2010

Ndugu Wananchi, Assalam Alaykum,

Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Subhana Wataala, aliyeumba mbingu na ardhi, kwa kutujaalia uhai na uzima tukaweza kuukaribisha mwaka 2011 Miladia na hivi karibuni tuliukaribisha mwaka 1432 Hijiria. Hiyo ni neema ya Mola wetu kuturehemu waja wake na hatuna budi kutoa shukurani kwake na kumuomba aujaalie mwaka mpya uwe wa kheri na baraka nyingi kwetu na kwa wengine wote duniani.

Kwa upande wangu naongeza shukurani za dhati kwa Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia fursa hii ya mwanzo kusalimiana na wananchi wenzangu na wengineo nikiwa Rais wa nchi yetu ya Zanzibar. Namuomba atujaalie sote maisha mazuri, afya njema na mafanikio katika malengo yetu ya maisha ya kila siku na ya baadae.

Ndugu Wananchi,

Tunamaliza mwaka ambao ulikuwa na matukio mengi makubwa nchini kwetu na nje ya nchi yetu. Katika mwaka huo tulikuwa na matukio makubwa manne. Kwanza tulipiga kura ya maoni ya Wazanzibari kujiamulia muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tulioitaka, hapo tarehe 31 Julai, 2010.

Katika kura hiyo ya maoni, asilimia 66.4 ya wananchi, iliafiki kuwepo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa. Tarehe 9 Agosit, 2010 Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walibadilisha Katiba ya Zanzibar kuingiza muundo huo katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Tarehe 31 Oktoba,2010 tulifanya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu mkubwa na mimi nikachaguliwa na wananchi wengi kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; baada ya kuteuliwa na Chama changu CCM, kugombea Urais. Kwa mara nyengine tena natoa shukurani zangu za dhati, kwa wote walioniunga mkono na kunichagua na wale ambao hawakuniunga mkono. Wote hao wametumia haki yao ya kidemokrasia.

Tarehe 3 Novemba, 2010, niliapishwa na kukabidhiwa rasmi madaraka ya kuiongoza Zanzibar. Baada ya hapo nilianza shughuli ya kuitekeleza Katiba kwa kumteua Mwanasheia Mkuu wa Serikali na baadae kuwateua Makamo wa Rais wa Kwanza na wa Pili pamoja na Mawaziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya muundo wa Umoja wa Kitaifa. Kadhalika niliwachagua Makatibu Wakuu na Manaibu wao kulizindua rasmi Baraza la Nane la Wawakilishi la Zanzibar, hapo tarehe 11 Novemba, 2010.

Ndugu Wananchi,

Baada ya muhtasari huo wa matukio makubwa ya kihistoria katika nchi yetu, nachukua nafasi hii kuzungumzia kwa ufupi yale tunayopaswa kuyazingatia na kuyafanya katika mwaka huu mpya na baadae, yenye maslahi kwa wananchi wote.

Natanguliza hoja ya kudumisha umoja, amani na utulivu, ambao umekuwapo tokea yale maridhiano ya Kihistoria ya Novemba 5, 2009 kati ya Rais Mstaafu Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, ambae sasa ni Makamo wa Kwanza wa Rais. Ni muhimu kwa wananchi wote, kuendeleza imani ya umoja wa Wazanzibari na moyo wa kukuza amani na utulivu.

Kutokana na hayo tutakuwa na nguvu na muelekeo mzuri wa kutekeleza mipango ya maendeleo ya nchi yetu, ambayo nitayazungumza katika sherehe za maadhimisho ya miaka 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964. Mengi niliyaeleza katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi.

Ndugu Wananchi,

Tunaingia katika mwaka mpya tukiwa tumepania kuijenga Zanzibar mpya yenye maendeleo na mafanikio. Sote kwa pamoja, kuanzia katika shehia, wadi, majimbo, wilayani, mikoani hadi taifa, tushirikiane katika kufanya yale tunayowajibika kufanya kwa mustakabali wa nchi yetu. Tukumbuke yale maneno ya Rais wa Marekani, John Kennedy aliyesema, tafsiri:

“Usiulize nchi yako itakufanyia nini, uliza nchi yako utaifanyia nini.”
Hivyo natilia mkazo uwajibikaji wa kila mtu; wafanyakazi, wafanyabiashara, wakulima, wavuvi, walimu, wanafunzi na kadhalika.

Tufahamu kuwa maendeleo ya nchi yetu, ya uchumi na ustawi wa huduma za jamii, utaletwa na sisi wenyewe. Washirika wetu wa Maendeleo watashirikiana nasi, pale watakapoona kwamba sisi wenyewe tunajitahidi. Kila mmoja wetu ana jukumu lake na mchango wa kutoa, hata kama ni kidogo, kwani wahenga wanasema, “Haba na haba hujaza kibaba”.

Ndugu Wananchi,

Katika ujumbe wangu huu, natilia mkazo haja ya kujenga imani, ya kujiamini, kuwa tunaweza. Tukumbuke msemo maarufu wa hayati baba wa Taifa, usemao “Inawezekana Timiza Wajibu Wako.”

Nina imani kubwa kwamba Wananchi wa Zanzibar tutaweza kuijenga Zanzibar mpya yenye neema. Mawaziri wangu wataeleza kwa kina malengo yetu ya maendeleo katika kutekeleza kazi zao. Wakati huo huo, nawasihi viongozi waliochaguliwa na wananchi yaani Wawakilishi, Wabunge na Madiwani, wawe wanatumia muda wao mwingi majimboni mwao, ili kutoa miongozo na ushirikiano na wananchi, katika utekelezaji wa mipango na miradi ya maendeleo katika shehia na wadi zao.

Madiwani washirikiane na masheha katika shughuli mbali mbali za maendeleo, zikiwemo usafi wa mazingira. Kufanya hivyo kutachangia katika kustawisha afya bora kwa wananchi.

Napenda kuelezea kwamba Zanzibar ni sehemu ya dunia. Nchi zote duniani zinakabiliwa na uchumi usiotabirika zaidi kutokana na kupanda kwa bei za mafuta. Ni bahati nzuri kuwa uchumi wetu katika kipindi cha awamu ya sita umekuwa ukipanda. Jukumu letu kubwa ni kutunza na kujali matumizi ambapo gharama za vitu mbali mbali hupanda kila siku kutokana na hali halisi ya uchumi wa dunia. Lazima tuzitunze na tuzitumie vyema rasilimali zetu. Tupige vita ubadhirifu.

Namalizia kwa kukutakieni nyote kheri na baraka za mwaka mpya 2011

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.