Habari za Punde

KWAHERI 2010 KARIBU 2011

Assalaamu Alaykum Waungwana

Kwa niaba ya blog yako ya Jikumbuke tunawashukuru wote waliobahatika kututembelea katika blog yetu ambayo kwa siku ya leo inatimiza miaka miwili tokea kuanzishwa kwake.

Msukumo wa kuendeleza kazi hii umetokana nanyi waungwana mnaotembelea, mnaotoa maoni, mnaohakiki, mnaotafuta, mnaofanya utafiti, mnaolaumu na kadhalika.

Katika kipindi hiki tumejifunza mengi kutoka kwenu na naamini nanyi mmefaidika japo kidogo katika kutembelea blog yenu ambayo imelenga zaidi katika kuwapatia habari, taarifa na matukio kwa picha ya yanayojiri katika visiwa vyetu vya Unguja na Pemba.

Kilichotusukuma ni kuona kwamba Visiwani ni wanahabari wachache wanaotumia blog katika kuhabarisha na ninachokifahamua si kwa kutaka bali kwa kukosekana nyenzo au vitendea kazi vya uhakika maana ukitaka kublog lazima uwe na Kompyuta ya uhakika (ambayo mimi sina) na uwe na internet ya uhakika vilevile (ambayo pia sinayo). Na kisha uwe na vianzio vya habari( ni vichache ninavyotegemea).

Hii ni kazi ya kujitolea ambayo haina tija wala mshahara hasa kwa vijiblog vyetu uchwara ambavyo si rahisi kuweza kuvitumia kama vitega uchumi kutokana na kuwa na traffic ndogo ya wazururaji a.k.a watembezi.

Kuna changamoto nyingi kama kwa watu wengi kuingia na kuchukua picha na taarifa bila ya hata kuomba idhini au angalau kutambua umuhimu wa kazi za wengine kwa kuweka blog yetu kama chanzo cha habari. Pia uchache wa teknolojia yenyewe ambayo hutukwaza kuweza kufanya mambo mengi na kadhalika

Tumeweza kupata maoni tofauti kwa wengine wanaopendelea zaidi picha kuliko habari, au kupendelea habari zaidi kuliko picha na wengine kutoa ushauri kwamba tuweke angalau na video kidogo ili wadau wapate uhalisia wa matukio kuliko picha mgando tu.

Kuna wengine wametushauri tuweke kibango cha kubadilisha pesa Foreign currency exchange rates na pia kutushauri kufikiria jina la blog kwamba haliendani na uhalisia wa mambo tutafute jina la asili ya Zanzibar na kadhalika.

Tunawashukuru wote na kuwatakia mwaka 2011 uwe ni mwaka wa mafanikio kwa sote katika kila tulikusudia nasi tutajitahidi kuendeleza jitihada hizi kwa msaada wenu kupitia maoni na kwa kututembelea na mkiona kimya kidogo pia mtuchukulie wakati mwengine huwa not reachable.

Wakatabahu

Othman Mapara

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.