Habari za Punde

ABDULHAMID HUMOUD KUJARIBIWA UTURUKI SOKA LA KULIPWA, BABI AUZWA RASMI

Jackson Odoyo

KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Simba, Adbulahim Homoud ‘Gaucho’ anatarajia kwenda nchini Uturuki kwa ajili ya kufanya majaribio wakati wowote kuanzia sasa.

Akizungumza na Mwananchi mjini Zanzibar kiungo huyo alisema mipango yake imeshakamilika na anachosubiri ni kupata baraka za viongozi wa Simba.

“Mipango ya kuondoka iko tayari kwa sababu vitu vya msingi vinavyohitajika vyote vimekamilika isipokuwa baraka ama ruksa kutoka kwa viongozi wa timu yangu ya Simba ndiyo nasubiri”alisema Homoud.

Alisema ingawa anakwenda kutafuta bahati ya kucheza soka la kulipwa kwa ajili ya maisha yake ya baadaye, lakini mapenzi yake katika soka la Tanzania bado yapo Simba na kamwe hilo hawezi kulificha.

Alisema anaamini kwamba viongozi wa Simba watakapo kaa na kujadili suala hilo watampa ruksa kwa sababu ni watu wanaoelewa na wanaopenda maendeleo ya kila mchezaji.

Pamoja na mchezaji huyo kusubiri baraka za viongozi wa timu hiyo bado hakuwa tayari kutaja majina ya timu ambazo anakwenda kufanyia majaribio nchini humo.

“Ni mapema sana kutaja jina la hizo timu ila ninachoweza kusema ni kwamba timu hizo zipo na mipango yote imeshakamilika hivyo muda ukifika nitawataarifu watanzania wote wafahamu,”alisema Homoud.

Hivi karibuni kiungo huyo alikuwa katika mgogoro wa kudai maslahi yake dhidi ya uongozi wa timu hiyo na hivi sasa mgogoro huo umemalizika na tayari ameshajiunga na kambi ya timu hiyo mjini hapa.

Wakati huohuo KLABU ya Dong Tam Long An ya Vietnam wamekubali kumnunua kiungo wa Yanga, Abdi Kassim 'Babi' kwa gharama ya dola za Kimarekani elfu 40 na anatarajia kuondoka nchini wiki hii.


Katika mazungumzo ya awali klabu hiyo ilitaka kumnunua mchezaji huyo kwa dola elfu 35, lakini Yanga waligoma na kutaka walipwe dola hizo 40 elfu ili waweze kumwachia mchezaji huyo.

Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema kuwa tayari wameshakubaliana na klabu hiyo na sasa bado kukamilika kwa mambo madogo madogo.

Alisema kuanzia leo watakuwa wakipeana mikataba ya pande zote mbili ili kila mmoja aweze kuisoma na kuielewa, lakini mambo yote yameisha na wameishatuma barua TFF ya kutaka watoe kibali chake cha kimataifa- ITC.

Alisema kuhusu maandalizi ya safari ya mchezaji huyo yamekamilika na viza ameshapata na wiki hii muda wowote anaondoka tayari kwa kuanza kazi katika timu yake mpya.
Chanzo: Mwananchi 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.