Habari za Punde

WAKIMBIZI WA KIZANZIBARI SOMALIA

 Mmoja katika wakimbizi wa Kizanzibari akijishughulisha na biashara ya mafuta
Wazanzibari walio ukimbizini  Mogadishu, Somalia wakiwa kwenye mazungumzo kwenye kiota chao

Wakimbizi wa kizanzibari waliopo Mogadishu nchini Somalia wamelalamikia matatizo mengi wanayokabiliana nayo kutoka kwa majeshi ya serikali pamoja na kikundi cha Al Shabaab.

Mmoja wa wakimbizi hao, Mohammed Said, wakati akihojiwa na Redio Shebelle alisema kwamba kuna takriban familia 85 ambazo zinaishi katika kambi ya wakimbizi iliyopo Hodan mojawapo ya miji iliyokumbwa na machafuko yanayoendelea nchini humo katika eneo la Benadir. Kwa mujibu wa kiongozi wa Wazanzibari, Ahmed Khatib kuna familia 192 za kizanzibari ambazo zimetawanyika katika miji tofauti nchini humo.

Aliendelea kusema kwamba wengi wa wakimbizi hujitafutia ajira angalau za kupata mlo au wengine hukimbilia kuwa omba omba kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili.

Licha ya jitihada zao kuomba misaada katika mashirika ya kimataifa ambayo yapo Somalia ila maombi yao hukataliwa kwa kutokuwa na hadhi ya ukimbizi (refugee status) na pia kwa kutokuwa na Serikali inayotambulika katika nchi hiyo na hivyo kuendelea kuishi katika mazingira magumu yanayotishia afya, pamoja na usalama wao.

Wakimbizi wa kizanzibari walikimbilia Somalia katika miaka 2001 wakati wa machafuko ya kisiasa yaliyotokea visiwa vya Unguja na Pemba na kutokea mauaji ya watu 27 na hivyo wengi wao walikimbilia kambi ya wakimbizi Shimoni, Mombasa Kenya na kisha wengine kuendelea mbele na kufika Somalia kwa kuhofia mahusiano mazuri kati ya Tanzania na Kenya wakihofia kurudishwa ambapo mpaka hii leo wanaishi maisha ya kikimbizi.

Walipofika Somalia miaka hiyo walipokelewa vizuri na wenyeji na kupewa moja ya majengo ya serikali kama makaazi yao ya kuishi na kusaidiwa chakula na mahitaji muhimu.

Baada ya muda, misaada ilianza kupungua na kuwafanya wengi wa wakimbizi wajitafutie njia za kujikimu ambapo wengi walianza kufanya kazi kama za kusomesha, uhunzi, useremala na uvuvi na wengine kuhamia miji mengine wakiendeleza biashara ya kukata nywele.

Kwa kuwepo muda mrefu katika nchi ya Somalia, wengi wa wakimbizi wameweza kujichanganya na jamii ya kisomali na tayari wameshaoa na kuzaa watoto ambao wanazungumza Kiswahili na kisomali na hawaoneshi kuwa tayari kurudi nchini mwao kwa kuwa na familia wanazopaswa kuzihudumia na huku wakiamini bado hali haijabadilika iliyowafanya waikimbie nchi yao miaka takriban tisa iliyopita.

Licha ya kujitokeza kwa kundi la Al Shabaab lenye msimamo mkali wazanzibari hao wanasema hawajapata kuhusishwa na vita hivyo na wala kubughudhiwa ila maisha yao kuwa roho juu kutokana na hali ya usalama kuwa ndogo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.