Habari za Punde

MAHAKAMA YAMWACHIA HURU MTOTO ALIYEDAIWA KUIBA BASKELI.

Na Khamis Amani

PAMOJA na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kumfikisha kizimbani mtoto wa miaka 16 kwa kosa la wizi wa baiskeli moja yenye thamani ya shilingi 90,000, hatimae Afisi hiyo yamuondolea shitaka hilo.

Afisi hiyo iliyoongozwa na Mwanasheria wake, Hamis Suweid, imemuondolea mtuhumiwa huyo shitaka hilo chini ya kifungu cha 100 (a) cha sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria za Zanzibar.

Mtuhumiwa wa kesi hiyo, Amar Said Haji (16) mkaazi wa Jangombe wilaya ya Mjini Unguja.
kabla ya kuondolewa kwa shitaka hilo, Mwanasheria huyo wa serikali kutoka Afisi ya DPP, aliwasilisha ombi hilo mbele ya hakimu Hamisa Suleiman Hemed ombi ambalo lilikubaliwa mahakamani hapo.

"Mheshimiwa shauri limekuja kwa ajili ya kusikilizwa, pamoja na hilo upande wa mashitaka tunaomba kuliondosha shauri hili chini ya kifungu cha 100 (a)", alisema Mwanasheria huyo.

Hakimu Hamisa Suleiman Hemed, alikubaliana na hoja hizo za upande wa mashitaka, na kumuondolea mtuhumiwa huyo shitaka hilo kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria.

Shauri hilo ambalo upelelezi wake ulikuwa tayari umeshakamilika, lakini upande wa mashitaka ulishindwa kuwasilisha mashahidi mahakamani hapo.

Hadi anaondolewa shitaka hilo, mtuhumiwa huyo alikuwa rumande kwa kukosa wadhamini.

Katika kesi hiyo kinyume na kifungu cha cha 267 (1) na 274 (1) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, mtuhumiwa huyo alidaiwa kuiba baiskeli moja aina ya Sehewa rangi ya silver yenye fremu namba E 10784 ikiwa na thamani ya shilingi 90,000 mali ya Ali Machano Mjomba.

Kabla ya wizi huo kinyume na kifungu cha 297 (1) (a) cha sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar, alidaiwa kuvunja nyumba anayoishi Ali Machano Mjomba na kuingia ndani kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi.

Matukio hayo yalidaiwa kutokea Kibweni Mchochani wilaya ya Magharibi Unguja, mchana wa Novemba 26 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.