Habari za Punde

TUHUMA KESI YA KUCHOMA MSAHAFU MAMIA WAFURIKA MAHAKAMA YA KWEREKWE.

Na Issa Mohammed

MAMIA ya waumini wa dini ya kiislamu wa mjini Zanzibar jana walifurika katika mahakama ya Mwanakwerekwe kusikiliza mwenendo wa kesi inayomkabili Ramadhani Handa Tuma anayetuhumiwa kuchoma moto msahafu mwezi uliopita.

Inadaiwa kwamba Tuma aliunguza msahafu huo katika eneo la Mombasa, nje kidogo ya mji wa Zanzibar hatua ambayo iliwakera waislamu ambao ni wengi ukilinganisha na waumini wa dini nyingine visiwani Unguja na Pemba.

Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga amethibitisha kufurika kwa waislamu hao wakiwa na hasira katika mahakama hiyo na kulazimika kuwatuliza kama njia ya kupunguza hasira walizokuwa zao.

Sheikh Soraga aliwaomba waislamu hao na wengine nchini kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambapo kesi hiyo inaendelea ili kuipa mahakama uhuru na kufikia maamuzi muafaka.

Akizungumza na waislamu hao nje ya viwanja vya mahakama, Sheikh Soraga alisema anaamini kwamba mahakama itatoa maamuzi yanayostahiki katika kuiendesha kesi hiyo ya aina yake hasa ikizingatiwa historia ya Zanzibar katika uislamu.

''Ndugu waislamu kuweni wavumilivu najua tukio la kuunguzwa moto msahafu limekuumizeni sana nyoyoni, lakini nina hakika haki itatendeka katika kuindesha kesi hii, nakuombeni kuweni wavumilivu, 'alisema Soraga

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 11 itakapotajwa tena katika mahakama hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.