Habari za Punde

UOZO ULIOACHWA UNAIKWAZA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA

Niliposoma taarifa za Uingereza ambapo mmoja katika wabunge wa zamani, David Chaytor amehukumiwa kwenda jela miezi kumi na nane kwa kutumia vibaya madaraka yake kwa kutumia zaidi ya Pauni 20,000 za walipa kodi katika matumizi binafsi; nilifurahishwa na jinsi utawala bora unavyotekelezwa kwa vitendo na si kwa mdomo na maslogan tu yasiyo mwanzo wala mwisho.

Akimhukumu, Jaji John Saunders,alimwambia, “huu ni hakika ni uvunjwaji wa uaminifu uliopewa kutokana na nafasi yako kama mbunge na hatimae umewekwa wazi na kukuaibisha. Na haya ndiyo matunda ya watu kama nyinyi mnaowania nafasi kubwa kubwa katika serikali na kuweza kupata hadhi na heshima na kisha kwenda kuwadhulumu wananchi ambao wamekuchagua”

Mheshimiwa Chaytor alidai alipwe Pauni 22,000.00 kama pango la nyumba, nyumba ilikuwa yake mwenyewe pamoja na mama yake, Alidai Pauni 1500.00 kwa huduma za IT (kompyuta) wakati huduma hii aliipata bila ya malipo.

Jaji hakutafuna maneno alimpa vidonge vyake kama vilivyo akimeza, akitema shauri yake.

Nikafikiria haraka nyumbani kwetu Unguja na Pemba ambapo vitu kama hivi ni vya kawaida mno kwa waheshimiwa kuunda safari zisizo na maelezo na kudai kulipwa pesa za walipa kodi kutoka serikalini.

Iliwahi kuripotiwa waheshimiwa wawakilishi wa baraza ililopita waliwahi kukataa kushiriki semina moja muhimu kwa sababu tu hakukuwa na vijisenti- allowance.

Na hapa ndio ninakuja kuamini kwamba serikali iliyopita ambayo hatuna budi kuisifu kwa kuleta maridhiano ila ilioza kwa kuwepo wezi, wabadhirifu wa pesa walipa kodi waliokuwa hawaogopi wala kuwa na khofu ya wakifanyacho kufikia hadi Serikali iliyoingia madarakani kuachiwa uozo ambao haujawahi kuachwa na Serikali zote zilizopita.

Serikali iliyopita iliweza kujenga tabaka la untouchables ambao ndio walikuwa wakitafuna pesa ya walipa kodi na wala hawakuweza kukaripiwa au kuambiwa chochote. Mfano mdogo mtu ka Katibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi anajiwa na Waziri na kuamriwa aidhinishe kutoa kiwanja, afanye nini naye ni mkubwa wake wa kazi? Likioza lawama zinamrudia katibu wakati waziri/mnene ameachwa untouchable. Anapoingia mtendaji mkuu wa nchi Makamo wa Pili wa Rais anshangazwa na kustushwa kwamba hivyo ndivyo nchi ilivyokuwa ikiendeshwa.

Baya zaidi ni pale Serikali inaposhindwa kufanya kazi yake kutokana na kutokuwepo miundo mbinu madhubuti mpaka Makamu wa Rais anahusika katika kutatua matatizo ya ardhi na chanzo chake ni mfumo mbovu wa madaraka na utawala usioheshimu sheria ya nchi wala utawala bora ambao kila mmoja wetu alikuwa na wajibu kufuata ila kwa untouchables walikuwa na haki ya kufanya watakalo.

Yote haya yanatendeka na hatujawahi kusikia kama kuna kiongozi yeyote wa ngazi za juu aliewekwa kiti moto kutokana na kutumia vibaya pesa za walipa kodi nani atamfunga paka kengele?. Balozi Seif Iddi una ubavu?

Tuliwahi kuhakikishiwa kwenye baraza letu tukufu lililopita kwamba Zanzibar hakuna Rushwa na aliyekuwa Waziri wa Afisi ya Rais, Fedha na hali halisi huko mitaani mwananchi wa kawaida ndiye anayekiona cha mtema kuni. Kufikia mtandao wa Wikileaks kututaja kwamba tunanuka kwa rushwa mpaka tunatazamwa lakini wala habari hatuna.

Kuna kijana wangu aliwahi kuajiriwa katika shirika moja kubwa la kiserikali kama mhasibu. MaashaAllah kijana alipata kidogo malezi na maadili. Katika wiki ya kwanza tu aliletewa cheki kusaini. Kama utaratibu alisaini. Siku ya pili aliletewa Milioni moja. Alipouliza za nini akaambiwa ahsante yako akaikataa kwani hajui kwa munasaba gani. Siku nyengine akaletewa cheki nyengine kusaini na baadae akaletewa milioni mbili mara hii ni bakhshish. Kazi ilimshinda katika kipindi cha mwezi mmoja aliandika barua ya kuacha. Waziri anasema hakuna rushwa, hakuna ubadhirifu. Watendaji wanachekelea na huku wanajiamini kwamba system inawalinda kwani hakuna kushitakiwa wala kutiwa hatiani.

Ulisikia habari za wale wahasibu waliokula pesa za serikali kwa kulipa wafanyakazi hewa na wengine wameshafariki na kugunduliwa mpaka hii leo nini kimeendelea? Jibu unalo mwenyewe.

Umesikia wale viongozi waandamizi wanavyopokea mishahara tofauti kwa majina tofauti ilhali ni huyo huyo na huku uchafu unaonekana lakini mhusika hagusiki – untouchable.

Tunapomsikia Makamu wa Rais anasisitiza kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria, sisi waandishi hutafsiri kwamba kuna tabaka ambalo limejiweka hivyo na tayari jamii imebidiishwa ikubali hali hii na matokeo yake tulikuwa na uongozi uliojaa uozo ambao serikali iliyopo imeonekana kukosa dira ya kujua hasa wapi ianzie katika kurekebisha uozo kwanza au kujikita katika kuleta maendeleo.

Kama Balozi Seif umeweza kufuta vibali, nenda mbali zaidi kwa kujua kama kuna mbinu zilitumika na wala usiunde tume wala kamati hatuna shida nazo tunataka vitendo vya papo kwa papo ndiyo njia pekee ya kufikisha ujumbe. Message received.

Ama kwa hili la uozo sina la kumsalia Mtume kwamba Serikali ya awamu ya sita ilitupeleka pabaya kupita awamu zilizotangulia.

Na Kitahanani bin Kitahayuri

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.