Habari za Punde

VIONGOZI WA SERIKALI WASHIRIKI MAZISHI YA SALUM JUMA OTHMAN

Na Rajab Mkasaba

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete leo aliongoza mazishi ya Waziri Mstaafu marehemu Salim Juma Othman aliyefariki dunia hapo jana katika hospitali Kuu ya MnaziMmoja mjini Zanzibar.

Katika mazishi hayo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi walihudhuria.

Mazishi hayo yalifanyika huko Shakani, Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama na Serikali pamoja na ndugu jamaa na marafiki wa marehemu na wananchi wengineo.

Marehemu Salim Juma Othman alistaafu Utumishi wa Serikali na Uongozi wa kisiasa mwaka 2005 baada ya kuitumikia Zanzibar na Tanzania Bara kwa miaka 31, na kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 59 katika hospitali ya MnaziMmoja ambako alilazwa kutokana na maradhi ya kisukari aliyokuwa nayo kwa muda mrefu.

Marehemu Salim Juma Othman alizaliwa tarehe 01.06.1952 katika kijiji cha Nanguji Kiwani Wilaya ya Mkoani Pemba.

Miongoni mwa nafasi za utumishi wake kisiasa katika maisha yake, Marehemu Salim Juma Othman kufuatia juhudi zake katika kazi za Chama na Utumishi wake mzuri na uadilifu katika kuwatumikia Wazanzibari na Watanzania kwa Jumla aliwahi kuwa Katibu wa CCM Idara ya Uenezi na Siasa Mkoa wa Kusini Pemba.

Aliwahi kuwa Katibu wa Wilaya wa CCM Kisarawe Mkoa wa Pwani Tanzania Bara na kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM) mwaka 1989-1991.

Mnamo mwaka 1991-1995 aliteuliwa kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na pia, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja mwaka 1995-1996.

Marehemu pia, aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Mjumbe wa Tume ya Jaji Warioba (Tume ya Kupambana na Rushwa), Mjumbe wa Tume ya Jaji Farancis Nyalali na pia kuteuliwa kuwa Makamo wa Mweneykiti wa Tume ya Jaji Kisanga ya kuratibu maoni ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano yaani(Whtite Paper).

Mnamo mwaka 1992-1994 Marehemu Salim Juma Othman aliteuliwa kuwa Kamishna wa Tueme ya Mipango. Aidha aliteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia aliteuliwa kuwa Mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kwa vipindi vitatu mfululizo.

Marehemu pia, alikuwa miongozi mwa Wajumbe wa Kamati ya makatibu Wakuu wa CCM na CUFkwa kuandaa na kuratibu Mwafaka wa kwanza na mwafaka wa pili baina ya mwaka 1992-2001.

Mwaka 1998 aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya kuratibu mapato ya Serikali

Mwaka 2000-2004 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Afisi ya Waziri Kiongozi na mwaka 2004-2005 aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na baadae kustaafu shughuli za siasa.

Marehemu Salim Juma Othman alijishughulisha na masuala ya kijamii na kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Zanzibar New Hope Society (DIASPORA), ambayo huwaunganisha Wazanzibari waliopo nje ya nchi wanaotaka kurudi nyumbani hadi yalipomfika mauti.

Marehemu Salim Juma Othman ameacha Kizuka mmoja na watoto sita na wajukuu watano.

Mapema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la mapinduzi Mhe. DK. Ali Mohamed Shein alikwenda nyumbani kwa marehemu kutoa mkono wa pole kwa kizuka pamoja na familia ya marehemu.

Dk. Shein aliungana na wananchi na wanafamilia na viongozi mbali mbali wa vyama na serikali kwa ajili ya kumsalia marehemu katika msikiti wa Mazrui Mombasa mjini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.