KUKAGUA wagonjwa ni Sunna nzuri ambayo imehimizwa na Bwana Mtume kuwa miongoni mwa mambo sita ambayo Muislamu yanamuwajibikia.
Wazanzibari wana bahati kubwa ya kulitekeleza jambo hilo tena kwa umakini mkubwa.Kwa msingi huo kwetu ni kitu cha kukizingatia sana kwa sababu wagonjwa sio wale tu waliolazwa hospitali na vituo vya afya bali hata walioko majumbani.
Jambo la kufurahisha na zuri linalofanywa katika kutekeleza wajibu huo ni yale makundi ya waumini ambayo hupita kwenye hospitali nyakati mbali mbali kwa kuwakagua na kuwaombea dua.
Lakini pamoja na wenzetu hao ambao wanafanya mambo mazuri kwa kuwaangalia wagonjwa mbali mbali na katika wodi mbali mbali, pia wapo wale wanaokwenda hospitali kumkagua mgonjwa maalum mmoja mmoja.
Hata hivyo, katika jambo hili zuri linalopaswa kuheshimiwa na kuigwa na kila mmoja wetu lakini pia kuna sehemu ya maudhi yanayofanywa na jamaa na marafiki wanaokwenda kuwakagua ndugu zao hospitali.
Hali hiyo isiyoridhisha hutokea zaidi katika kipindi cha jioni cha kukagua wagonjwa, ambapo ndugu zetu wakike hujitokeza kwa wingi.Kitu ambacho mimi huwa hakinifurahishi ni kuwaona kinadada wakitumia manukato ya hali ya juu wanapokwenda hospitali kuwakagua.wagonjwa.
Kwa upande mmoja ni kitu muhimu chenye kheri na baraka tele lakini kwa upande mwengine kinakuwa kama bughudha kwa wagonjwa ambao hali zao huwa mbaya na hawajisikii raha.Wapo wanaojitwisha manukato ya hali ya juu, wengine wakivaa nguo za fahari sana na wengine huvaa mapambo makubwa makubwa mwilini mwao.
Ingawa hakuna kinachokatazwa lakini kinachofanyika sinahakika kama ni miongoni mwa adabu za kiislamu, lakini mtu kujivalisha mavazi kama hayo ni vyema basi akafanya anapokuwa nyumbani kwake na mumewe badala ya kuvaa akiwa nje ya nyumba yake.
Urembo, Utaarazi na mapambo hayakatazwi lakini ni bora yavaliwe katika sehemu zifaazo yaani majumbani na sio hospitali kwa sababu kufanya hivyo ni jambo la karaha kidogo kwa wagonjwa.
Aziza R.A. Mohammed
Mbuyu Pacha,
Zanzibar
Tujaribu kuongelea Waislam kwa ujumla sio kila mara Wazanzibari; Hakuna dini inayoitwa Wazanzibari, huu ni ubaguzi wa kijamii na Uislam hauruhusu ubaguzi wa aina yoyote ile...
ReplyDelete