Habari za Punde

SERIKALI IFIKIRIE UJENZI WA MIJI MIPYA

Salum Vuai, Maelezo

KATIKA nchi zilizoendelea na zile zinazopiga hatua kwenda mbele, utaratibu wa kuanzisha miji mipya ni jambo linalopewa kipaumbele.Kwa vile kukua kwa miji kunatokana na ongezeko la watu, na kwa kuwa wote hao hawawezi kuishi katika sehemu za miji, ndipo serikali hizo zinapokuwa na mikakati endelevu ya kujenga miji mipya.

Mikakati hiyo huandaliwa kitaalamu kwa kushirikisha kila sekta kama vile mamlaka za ardhi na zile zinazoshughulikia mazingira, afya, maji, huduma za umeme, elimu na mambo mengine muhimu kwa jamii.
Sekta zote hizo zina sehemu katika kufanikisha maendeleo ya miji na kwa hivyo kila moja hutoa mchango wake wakati wa upangaji miji hiyo.

Katika hili, serikali hutenga maeneo mapya kwa ajili ya ujenzi wa makaazi ya wananchi wake, na huduma zote hizo hufikishwa kwanza pamoja na kutenga viwanja vya skuli, vituo ya afya, maeneo ya nyumba za ibada, masoko pamoja na viwanja vya wazi kwa ajili ya michezo.

Hatua hii inalenga kuyaweka tayari maeneo hayo na pale wananchi wanapogaiwa viwanja na kujenga nyumba za makaazi, hawapati shida kufikisha huduma za maji na umeme ndani ya nyumba zao.

Kwa mpango huu, kunakuwa hakuna sababu kwa watu wanaotaka kuanza maisha mapya kung’ang’ania kubaki mijini hata pale miji hiyo inapoonekana kuelemewa na idadi kubwa ya wakaazi.

Kukosekana kwa utaratibu kama huu hapa nchini, ndipo kunapojitokeza msongamano mkubwa kwani kila mmoja anaona mji mkuu ndipo pahala pazuri pa kujiajiri na hivyo biashara kutamakani kila pembe hata vichochoroni.

Baraza la Manispaa hapa Zanzibar linakabiliwa na kazi ngumu kufukuzana na vijana wanaoamua kujiajiri japo kwa biashara za mikononi, kwani hakuna maeneo mbadala yaliyokuwa tayari na ambayo yana kila mahitaji yatakayoweza kuwafanya wananchi hao wakubali kuishi huko na kuendesha maisha yao kwa utulivu.

Tunashukuru serikali imeanza kuchukua hatua kwa kugawa viwanja na kutenga maeneo kwa huduma muhimu huko Tunguu, ambako ujenzi unaendelea kwa kasi.

Ili kupunguza msongamano katika Manispaa, ni vyema mpango huu ukaendelea kwa kuangalia maeneo mengine ambayo bado hayajafikiwa kwa ujenzi kama huo.

Tunguu ni kwa upande wa Kusini, sasa iko haja kutanua wigo hadi njia ya kati ipitayo Mwera na vijiji jirani pamoja na mkoa wa Kaskazini.

Pamoja na kuwa katika maeneo hayo asilimia kubwa ni ardhi ya kilimo, lakini nina hakika kama serikali itaamua basi haitakosa maeneo mazuri kwa ujenzi.

Dawa mjarabu ya kumaliza msongamano mjini ni kuanzisha mfumo wa ujenzi wa miji mipya na uendeshwe kitaalamu na pia uepuke urasimu.

Jambo hili pia linataka dhamira na uwajibikaji kwa wale wanaokabidhiwa majukumu, wafanye kazi kwa ushirikiano ili kufikia malengo yanayokusudiwa.Mbona wenzetu wameweza kuongeza miji na maisha yanakwenda vizuri huku vijana wengi wakitawanyika katika maeneo mapya na kuendesha biashara na ajira nyengine?

Kipi kinatukwamisha sisi, ni ukosefu wa fedha, uvivu wa kufikiri, au kukosa nia njema katika kuiendeleza nchi yetu?

Lazima tufike pahala tuache kuhusudu wenzetu wa nchi nyengine walivyofanikiwa kama tulivyozoea ambapo wale wanaobahatika kutembelea nchi hizo wanaporudi nchini hutusifia jinsi nchi hizo zilivyopiga hatua.

Nadhani badala ya kukaa na kuwasifu wenzetu, tutumie ziara tunazofanya ng’ambo kujifunza na kuiga kwa vitendo kwani hakuna ubaya katika kumkopia mwenzako aliyefanya vyema na kupata mafanikio.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.