Na Mwandishi wetu
BEI ya mafuta imepanda katika visiwa vya Unguja na Pemba na kuongeza ukali zaidi wa maisha kwa bidhaa nyengine kufuata mkondo.
Katika vituo vya kuuzia mafuta, bei ya petroli inauzwa kwa shilingi 1,870 kutoka shilingi 1,735, ambako kuna ongezeko la shilingi 135 kwa kila lita moja.
Bei ya dizeli inauzwa kwa shilingi 1930 kutoka shilingi 1755, ambapo kuna tofauti ya shilingi 175.
Uchunguzi wa gazeti hili umegundua kwamba biashara hiyo pia haipatikani katika vituo vingi vya kuuzia mafuta huku vile vichache vinavyotoa huduma vikiwa na foleni kubwa za vyombo vya moto na watu wanaonunua huduma hiyo kwenye madumu.
Aidha uchunguzi huo umegundua mafuta yamekuwa yakiuzwa zaidi kwa walanguzi ambao nao huuza kwa bei ya juu kwa shilingi 3000 kwa lita ya petroli na shilingi 3200 kwa lita ya dizeli.
Kulikuwa na idadi kubwa ya walanguzi katika kituo cha kuuzia mafuta Kariakoo, ambapo licha ya mafuta kuuzwa kituoni, pia walanguzi wamekuwa wakiuza bidhaa hiyo kwa wateja wasiotaka usumbufu mita chache tu kutoka kituoni hapo.
Katika kituo cha mafuta cha jirani, hakukuwa na shughuli zozote ambapo mwandishi wa habari hizi aliambiwa kuwa kituo hicho kilikuwa hakina mafuta.
Licha ya huduma ya mafuta kupanda, mwandishi wa habari hizi alishuhudia lori la mafuta likijaza mafuta katika moja ya matangi yaliyopo katika kituo cha kuuzia mafuta cha Kariakoo hali ambayo inaashiria bidhaa hiyo bado ipo katika maghala ya kuhifadhia.
Kulikuwa na misururu mikubwa ya magari na vyombo vyengine vya moto vilivyokuwa vikihitaji huduma ya mafuta katika kituo cha Gapco.
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya wateja wamesema kuwa mafuta bado hayajaadimika lakini wafanyabiashara wamekuwa wakipandisha bei kwa makusudi.
Walisema hali hiyo imekuwa ikiwaumiza wananchi hasa wa kipato cha chini ambao wamekuwa wakitegemea huduma ya mafuta kwa shughuli zao mbali mbali.
Serikali bado haijasema lolote kuhusiana na kupanda kwa bei ya mafuta huku jamii ikiamini kwamba bado kuna akiba kubwa ya mafuta katika hifadhi ya serikali Mtoni.
Kwa Tanzania Bara bei za nauli za magari imepanda, ambapo nauli ya chini kwa sasa ni shilingi 300 kutoka shilingi 250.
Kupanda kwa bei ya mafuta sasa kutawafanya wamiliki wa vyombo vya usafiri kupandisha nauli, ambapo kwa upande wa kisiwa cha Pemba tayari nauli za vyombo vya usafiri imepanda.
Hali hiyo imesababishwa na maandamano yanayoendelea katika nchi za Kiarabu na Mashariki ya Kati, ikiwemo Libya ambayo ni nchi ya 13 kwa uzalishaji wa mafuta duniani.
Ingawa Libya haiathiri sana soko la bidhaa ya mafuta, lakini mafuta yake yamekuwa yakipendwa zaidi na watumiaji.
Tatizo jengine ni kuongezeka kwa uharamia katika pwani ya bahari ya Hindi ambapo meli za mafuta hulazimika kusafiri masafa marefu zaidi kuwakimbia maharamia hao.
Katika soko la dunia, bei ya mafuta yasiyosafishwa yamekuwa yakiuzwa kwa dola 119 za Marekani kutoka dola 75 kabla ya kuibuka kwa mgogoro Afrika Kaskazini.
Kwa mujibu wa Shirika la Usafirishaji mafuta (OPEC) usambazaji wa bidhaa huenda ukapanda zaidi katika siku za usoni.
Makampuni mengi yamesimamisha kutoa huduma nchini Libya na nyengine zimeanza kuwaondoa wafanyakazi wake nchini humo
No comments:
Post a Comment