Na Sad Abdul-rahman Pemba
TIMU ya Kivumbi kutoka Raha hapo jana ilijinyakulia point 3 muhimu baada ya kuifunga timu ya Kichungwa kutoka Chasasa Wete kwa jumla ya mabao 3-2 katika mchezo wa ligi daraja la pili Wilaya ya Wete kisiwani Pemba.
Mchezo huo ambao ulipigwa katika dimba la uwanja wa Kinyasini wakati wa saa 8:30 za mchana ambapo mabingwa hao ndio wa mwanzo kuziona nyavu za mahasimu wao hao kwani jana walikuwa ni kama mboga tu kwao.
Mnamo dakika ya 14 tu tokea kuanza kwa mtanange huo timu ya kivumbi waliweza kuandika bao kupitia kwa mchezaji wake Ali Juma Ali na huku kichungwani wakirejesha bao hilo mnamo dakika ya 20 ya kipindi hicho cha kwanza kupitia kwa mchezaji wake Maulid Khamis.
Hata hivyo kichungwa walijitutumua na kuweza kupata bao la pili lililofungwa na mchezaji Juma Khamis mnamo dakika ya 60 ya mchezo huo.
Kuingia kwa bao hilo kivumbi walikuja juu mithili ya moto wa kifuu na kufanikiwa kupata bao la kurejesha mnamo dakika ya 72 kupitia kwa mchezaji wake Salum Said Ali na yeye ndie aliemaliza karamu hiyo ya magoli mnamo dakika ya 85 alipoweza kuandika bao la tatu na la ushindi katika mchezo huo.
Na katika michezo mengine iliyopingwa hapo jana ni kuwa Mkwajuni waliweza kuifunga timu ya Stone town kwa jumla ya mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa katika kiwanja cha Skuli ya Utaani,huku Hindi wakigawana ponti moja moja na timu ya Ranger boys ambapo mchezo huo ulipigwa katika dimba la uwanja wa Msaani.
Wakati huo huo wageni wa ligi kuu Zanzibar timu ya Madungu hapo jana walijikuta wakigawana point 1-1 na timu ya Duma ambayo inamilikiwa na jeshi la kujenga Uchumi (JKU) Kisiwani Pemba baada ya timu hizo kutoka sare ya kufungana mabao 2-2 katika mchezo uliopigwa katika uga wa uwanja wa Kinyasini.
Mabao ya wageni hao yaliweza kuwekwa kimiani na Rashidi Juma Habibu katika dakika ya 15 na Vuai Abdalla katika dakika ya 85 ya mchezo huo.
Na huku mabao ya Duma yaliweza kuwekwa wavuni na SalumNassor katika dakika ya 29 na Ali Ame ambae ni mrithi wa mchezaji Ali Shiboli aliekimbilia Simba ya Dar-es-salaam, mnamo dakika ya 49 ya mchezo huo.
No comments:
Post a Comment