Na Rajab Mkasaba
WAISLAMU nchini wametakiwa kuifanya misikiti iwe kwa dhamira za kuendeshea ibada na kuendeleza manufaa ya elimu ya dini na mambo mengine ya kheri ikiwa ni pamoja na kusomeshea darasa za dini na kuwasomesha watoto.
Hayo yameelezwa leo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein mara baada ya ufunguzi wa msikiti wa Masjid Taqwa uliopo Dimani Bondeni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika maelezo yake Alhaj Dk. Shein amewasisitiza Waislamu wa eneo hilo la Dimani wasikubali kwa hali yotote kubaguana katika hayo na kama walivyoshirikiana katika kuujenga msikiti huo basi wasikubali kugawanywa katika uendeshaji na usimamizi wake.
Alielezaa kuwa MwenyeziMungu na Mtume wake Mohammad (S.A.W), hawakuelekeza Waislamu kugombana kwa ajili ya kugombania uongozi wa msikiti bali viongozi huchaguliwa na watu ambao ndio wenyewe waumini wa dini ya Kislamu.
Alhaj Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa misikiti ni kielelezo thabiti cha imani ya Waislam kwa Mola wao na dini yao kwa ujumla na kusisitiza kuwa Mwenyezi Mungu amewasifu wanaojenga na kuimarisha misikiti kuwa ni waumini wa kweli na Mtume Muhammad (S.A.W), amethibitisha malipo mema juu yao.
Akinukuu aya ya 18 ya Suratul Jinni, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa ‘Na hakika Misikiti ni ya MwenyeziMungu basi msimuabudu yeyote pamoja na MwenyeziMungu”. Pia alinukuu kauli ya Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) kuwa “Anaejenga msikiti kwa ajili ya MwenyeziMungu basi MwenyeziMungu atamjengea nyumba peponi”.
Aidha, Dk. Shein alitoa wito kwa Waislamu kuwa wasikubali kugawanywa katika dhana zisizo njema kuwa kuna ubora wa misiki na kusihi kuwa misikiti yoye ni ya MwenyeziMungu na yote ni mitukufu hivyo haifai kudharauliwa.
Alisema kuwa Misikiti iliyotajwa kwa utukufu, ubora zaidi ni Msikiti Mtukufu wa Makka (Masjid Haram), Msikiti Mtukufu wa Mtume Madina (Masjid Nabawi) na Msikiti Mtukufu wa Al Quds uliopo Jerusalem.
Alhaj Dk. Shein alisisitiza suala la kusomeshwa Qur-an na kuwataka wale wote wenye elimu hiyo kuwasaidia wenzao ambao hawana elimu hiyo ili Zanzibar iendeleze historia yake juu ya elimu ya Qur-an. “Hakuna mbadala wa Qur-an kwani ni uongofu wetu”,alisisitiza Alhaj Dk. Shein
Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa shukurani kwa wafadhili wote waliofadhili, waliosaidia ujenzi wa msikiti huo na kuwatakia kila la kheri kwa MwenyeziMungu Waislamu wote wa kijiji cha Dimani na wengineo waliotumia nguvu zao na mali zao na hata mawazo na busara katika kufanikisha azma ya kuhakikisha wanashirikiana vyema na wafadhili katika kuukamilisha msikiti huo.
Akisoma taarifa fupi ya ujenzi wa msikiti huo, Maalim Juma Wakili alisema kuwa ujenzi wa msikiti huo ulianza Agosti 2010 mpaka kumalizika umegharimu jumla ya Shilingi Milioni 75 za Kitanzania.
Alieleza kuwa kabla ya hapo msikiti uliokuwepo ulikuwa mdogo na usiokuwa na mazingira mazuri na kwa vile kijiji kina kuwa siku hadi siku pia wana malengo ya kusali sala ya Ijumaa na sala ya Idd hapo baadae katika msikiti wao huo mpya sanjari na kutoopata nafasi kwa ajili ya kuendesha darsa kwa watu wazima na vijana wadogo ndani ya msikiti.
Pia, Maalim Juma alieleza kuwa hivi sasa vijana wengi wa Kizanzibari wanamomonyoka kimaadili kwa kujiingiza katika mambo mbali mbali yasiofaa hiyo ni kutokana na kukosa elimu ya dini yao ya Kiislamu.
Alitoa wito kwa wazazi na Waislamu wote kwa ujula kushirikiana na kuweka mikakati madhubuti ili kuwanusuru vijana wa Kizanzibari na Taifa kwa jumla.
Aidha, Waislamu hao wa kijiji cha Dimani waliunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na madawa ya kulevya na kuomba juhudi hizo ziendelee ili kuondosha na maovu mengine yote.
Akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khamis Haji alitoa shukurani kwa wafadhali wa msikiti huo, waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na viongozi wa Jimbo hilo la Dimani kwa kushirikiana pamoja katika ujenzi wa msikiti huo na kutoa shukurani kwa Alhaj Dk. Shein kwa kushirikiana nao pamoja.
Mapema Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Soraga akitoa hutuba ya sala ya Ijumaa, alitoa wito kwa Waislamu kuwa misikiti iwe kitovu cha mafundisho ya Uislamu na kuitaka Kamati ya msikiti huo kuwa madhubuti kutokana na matukio mbali mbali yanayojitokeza katika misikiti hapa nchini juu ya suala zima la kugombania uongozi wa misikitini.
Viongozi mbali mbali wa dini, vyama na serikali pamoja na wananchi wa Dimani walihudhuria katika ufunguzi huo wa msikiti huo.
No comments:
Post a Comment