Wasema itawafanya wajitume, kuacha kusinzia Barazani
Na Haroub Hussein
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar kuanzisha kanuni maalum za adhabu ambazo zitakayoweza kumuadhibu Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi ambaye atashindwa kutoa mchango wowote wakati wa vikao vya Baraza hilo vikiendelea.
Ushauri huo umetolewa wanasiasa katika Kongamano la kutathmini Uchaguzi Mkuu wa 2010, lililofanyika katika hoteli ya Zanzibar Ocean View iliyopo Kilimani mjini hapa.
Akichangia katika Kongamano hilo Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha TADEA, Ali Mohammed Mbongo alisema kutungwa kwa kanuni hiyo kutawafanya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kujituma na kuwasilisha mawazo ya wananchi ambao ndio waliowapa ajira.
"Kutochangia katika vikao vya Baraza kwa kipindi chote cha miaka mitano ni aibu pia ni kuwanyima fursa wananchi waliokuchagua katika jimbo lako, hivyo kutungwa kwa kanuni kutasaidia sana kuwafanya wale wanaofika Barazani na kusinzia kuacha kufanya hivyo kwa kuogopa kuadhibiwa", alisema Naibu huyo.
Aidha alisema katika Baraza la Wawakilishi utakuta Mwakilishi anawatetea wananchi wa jimbo ambalo si lake wakati Mwakilishi wa jimbo husika yupo huku akiwa amenyamaza kimya jambo linalowanyima fursa wananchi hao ya kutowakilishwa vizuri kwenye chombo hicho cha kutunga sheria.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha TADEA, Juma Ali Khatib,alisema sheria ya kuwapa Wawakilishi na Wabunge viinua mgongo vikubwa inarejesha nyuma na kufanya kiwango cha mabadiliko kuwa kidogo kwa kupelekea wastaafu hao wa kutunga sheria kutoa rushwa katika majimbo na kurudi tena.
Aidha aliitaka ZEC kupitia ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuishauri serikali kurudisha utaratibu wa kutoa ruzuku kwa vyama vyote ili kuweka usawa katika uchaguzi wa 2015.
Nae Mwenyekiti wa Chama cha wakulima AFP Said Soud Said, aliitaka serikali kufuata sheria inayoitaka kutoa asilimia moja ya mapato yake kwa Tume ya Uchaguzi(ZEC) ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi,jambo ambalo kwa sasa halipo na kuvifanya vyama vya siasa kuilaumu Tume hiyo.
Kwa upande wake Rashid Mshenga kutoka AFP, alitaka kuwepo sheria itakayoiwezesha Tume kumiliki viwanja vyote wakati wa kampeni za uchaguzi, badala ya Mkuu wa wilaya ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
No comments:
Post a Comment