CHAMA cha Soka Zanzibar (ZFA) Wilaya ya Mjini, kimeendelea kuonesha makali dhidi ya wachezaji wanaokiuka maadili ya michezo kwa kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu.
Katika hatua ya hivi karibuni, chama hicho kimetangaza kumfungia mchezaji wa timu ya Sicco Vuai Suluhu Ame kutoshuka dimbani kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kumpata na hatia ya kumpiga muamuzi.
Mchezaji huyo anadaiwa kumpiga muamuzi Mfaume Ali na kumsababishia maumivu juzi Jumamosi wakati timu yake ilipocheza na Mwembeladu katika ligi ya soka daraja la pili. .
Barua ya chama hicho iliyosainiwa na Katibu wake Yahya Juma Ali, imefahamisha kuwa kitendo alichofanya mchezaji huyo, hakiwezi kufumbiwa macho kwani kinakwenda kinyume na kanuni ya mashindano ya ligi Zanzibar kifungu namba 15 na 24.
Sambamba na adhabu hiyo, ZFA pia imeipiga faini ya shilingi laki moja timu yake, na kutakiwa ilipe si zaidi ya Machi 23 mwaka huu.
Katika hatua nyengine, chama hicho kimemfungia kiongozi wa timu ya Taifa Jipya Salum Mohammed Kingwasa kutohudhuria mechi yoyote ya timu yake kwa muda wa miezi sita pamoja na wachezaji watatu wa timu hiyo.
Wachezaji hao ni Juma Mbarouk, Suleiman Said na Issa Hamad, ambao wote wanadaiwa kumshambulia muamuzi wakati timu yao ilipocheza na Tottenham.
Timu hiyo pia imepigwa faini ya shilingi laki mbili ilizoamriwa kulipa si zaidi ya kesho pamoja na kupoteza ushindi, huku Tottenham ikizawadiwa ushindi wa magoli mawili na pointi tatu
No comments:
Post a Comment