Habari za Punde

ZANZIBAR IMEJIANDAA VIPI NA TSUNAMI?

A K K Simai

Hivi karibuni tumeshuhudia katika vyombo vya habari madhara makubwa yaliyotokea Japan kutokana na mtetemeko mkubwa wa Ardhi pamoja na Tsunami. Maelfu ya watu wamefariki na wengine bado hawajulikani hatima yao kutokana na mawimbi makubwa yenye kina cha mita kumi kufika ardhini kwa kasi na kuharibu kila kilichosimama.

Madhara makubwa yametokea katika mji wa Sendai kaskazini mashariki mwa Japan na sehemu nyingi ambazo zipo kando kando na bahari zimeathirika vibaya sana kutokana na Tsunami. Waziri Mkuu wa Japan ameliweka tukio hili sawa na yaliyotokea takriban miaka 60 iliyopita Vita vya pili vya Dunia.

Japan ni nchi iliyoendelea. Iliwahi kukumbwa na Tsunami 1920 ambapo watu 120,000.00 walifariki. Japan ni nchi iliyopo katika mkanda wa ardhi ambao hutokea matetemeko mengi ya Ardhi na imejiandaa kadri ya uwezo wake kukabiliana na majanga ya aina hii.

Licha ya ukubwa wa mtetemeko katika kipimo cha Richter (Richter scale) 8.9, hatukuona nyumba zilizoanguka kutokana na mtetemeko (zilizoanguka zilikumbwa na dhoruba ya tsunami) wakati majuzi tu New Zealand ilipata mtetemeko ambao ni maradufu kulinganisha na Japan lakini nyumba nyingi ziliharibiwa. Japan inajenga nyumba zake quake proof (tayari zina hifadhi na mitetemeko)

Zanzibar si mgeni wa majanga lakini nina imani Mola wetu anatupa yetu kutokana na hali zetu ‘dhooful haal’. Mwaka 2009 tulipata mtihani wa kuzama meli Mv Fatih wakati ikijaribu kutia nanga bandarini. Meli ilichukua muda mrefu kuopolewa tena kwa msaada kutoka Tanganyika. Watu sita walifariki. Tume iliundwa na ikaleta ripoti. Mapendekezo yalifanyiwa kazi Kwani hatukuwa na Tagi lenye winchi nzito ya kuweza kuibeba Meli na Jitihada nyingi za kienyeji zilizokosa utaalamu zilijaribiwa na kufeli.

Mwaka 2009 huo kuna meli mbili pacha zilikuwa matengezoni Mtoni Mv Aziza 1+2, nazo zilishika moto. Vikosi vya zimamoto viliitwa kudhibiti hali kwa kuwa Meli zilikuwa karibu na ufukwe. Je ikitokea Meli kuwaka na iko nangani tuna kifaa chochote cha kuweza kuzima moto baharini?

Mwaka 2005 kulitokea mvua kubwa za El Nino. Maeneo mengi yalijaa maji na nyumba nyingi kuharibika katika maeneo ya Kwahani, Sebulani, Kwamtipura na kadhalika.

Mawimbi ya Tsunami yanaweza kutembea masafa marefu na kwa kasi na kuweza kuathiri sehemu nyengine ambazo hazipati mtetemeko wa lakini zinaweza kupata athari za Tsunami kama ilivyotokea mwaka 2006 Kusini mashariki mwa Asia ambapo mawimbi yaliweza kufika mpaka fukwe za Somalia, Kenya na kadhalika.

Ulimwengu hutoa tahadhari ‘alert’ ya kujuulisha kuwepo kwa tsunami. Ingawa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi wanaoishi katika mwambao wa Bahari ya Hindi kuondoa wasiwasi wa kukumbwa na hali hiyo, hivyo wanapaswa kuendelea na shughuli zao ila suala la kimsingi endapo hali hii itatokea wananchi tayari wameshaelimishwa (awareness) nini wanatakiwa kufanya? Je vipi idara yetu ya hali ya hewa ina utaratibu wowote wa kupokea hizi tahadhari na huzifanyia kazi angalau kuwatahadharisha wananchi, wavuvi, wasafiri ambao hutumia bahari?

Kuna mazoezi yoyote yaliyowahi kufanyika kama “drill” ambayo yangelioneshwa kwa televisheni zetu vipi mwananchi akiwa baharini, nchi kavu, kando kando mwa bahari anatakiwa afanye? Japan kukitokea mtetemko, kila mwananchi anajua nini afanye vipi ajipange katika kuikabili hali hii.Kuna matangazo yoyote au vipeperushi vilivyoandaliwa ambavyo vinatoa taarifa na maelekezo likitokea janga la tsunami nini wananchi wafanye?

Na vipi hiyo taarifa ya tahadhari itaweza kutolewa kwa kutumia njia gani, redio, Tv, simu, mdomo kwa mdomo pasipo kuleta kuhamanika (panic) na kitahanani kwa wananchi na kwa muda wa haraka na hapa ndipo panapohitaji maandalizi na mipangilio.

Zanzibar ni nchi masikini. Lakini umasikini wetu usiwe kigezo cha kukosa maandalizi angalau kwa kadri ya uwezo wote na hili tusisubiri wafadhili waje kutusaidia ili kukitokea majanga au maafa tuweze kujipanga.Umasikini wetu usiwe sababu ya kutukwaza katika mambo ambayo yataweza kuokoa maisha ya watu hasa ukizingatia mazingira ya kisiwa chetu jinsi kilivyo takriban sawa na usawa wa bahari kwa maeneo mengi. Wimbi la mita tano tu likija kwa nguvu ya tsunami basi nusu ya mji wa Zanzibar upo majini. Madhara yake ni Allah pekee anayejua.

Tusisubiri yatokee kisha tuanze kuunda tume, tuwe ‘proactive’ wabunifu kabla ya majanga na maafa na huku ndiko kujiandaa tunakoshauri vyombo husika kama Tume ya Maafa na kadhalika hasa kwa majanga ambayo yanaweza kutukabili katika maeneo yetu kutokana na hali halisi ya kiulimwengu na mabadiliko ya hali ya hewa.

Ndiyo tuna matatizo mengi na hili la tsunami si la kutuumiza vichwa kama baadhi yetu wakatakavyotumia hoja ya kudadisi haja ya kujiandaa na tukio hili la ‘kufikirika’ Ila msemo wetu wa Kiswahili unatukumbusha ‘mwenzako akinyolewa...

Tumuombe Mola wetu atuepushe na majanga na maafa kwa rehma na nguvu zake Subhaana.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.