Na Halima Abdalla
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana kimeichoma moto rasimu ya Mswada wa uandaaji wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuashiria kuukataa moja kwa moja, kama inavyoonekana pichani.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Chama hicho huko Kibandamaiti Mjini Zanzibar jana, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, Hamad Mussa Yussuph, alisema Mswada huo wameamua kuuchoma kutokana na kuuleta Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Walisema Waziri Sitta ndie aliyeongoza Bungeni kupitisha uamuzi wa Rais wa Zanzibar kuondoshwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kipindi alichokuwa waziri wa Sheria.
Alisema mabadiliko ya 11 ya Katiba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndio yaliopelekea Rais wa Zanzibar kupoteza nafasi kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, ambayo ilipitishwa na Waziri Sitta bungeni akiwa Waziri wa Sheria wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha alimuomba Rais wa Zanzibar kupitisha kura ya maoni kwa wananchi wa Zanzibar kuhusiana na rasimu hiyo ya Katiba, ili wananchi wa Zanzibar watoe maoni yao.
Aliiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutokubali kupokea rushwa katika kushawishika kuikubali rasimu hiyo ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa Upande wake mwanaharakati wa kutetea Zanzibar, Ali Omar Juma, alisema wananchi wa Zanzibar tayari wameshapeleka notisi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon kutoikubali rasimu hiyo.
Alisema wananchi wa Zanzibar wako tayari kuishtaki Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mahkama ya kimataifa, iwapo itapitisha mswada huo wa Katiba mpya.
Alisema rasimu hiyo iliyoletwa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yeyote atakaekubali haitakii mema Zanzibar.
Toka tumeungana na Tanganyika tumekuwa watumwa wa Tanganyika,''alisema Mwanaharakati huyo.
Mkutano huo wa CHADEMA ulipata baraka za kuhudhuriwa na wananchi wa vyama mbali mbali, kutokana na kuwa wa kwanza tokea kufanyika mikutano miwili mikubwa ya kujadili rasimu hiyo iliyowasilishwa na kamati ya katiba na Sheria ya Bunge la jamhuri ya Muungano wa tanzania, ambapo mkutano wa pili ulishindwa kufikia tamati baada ya kuzuka ghasia kwenye ukumbi wa skuli ya Sekondari ya Haiele Sellassie juzi.
No comments:
Post a Comment