Habari za Punde

FUONI WATAKA UTEKELEZAJI WA AHADI ZA VIONGOZI

Na Ismail Mwinyi

WANANCHI wa Fuoni Kibonde mzungu Wilaya ya Magharibi Unguja, wamewataka viongozi wa jimbo lao kutekeleza ahadi zao walizoahidi wananchi wakati wa kipindi cha kampeni ili kuleta mabadiliko ndani ya jimbo hilo.

Wakizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao, baadhi ya wananchi hao walisema tangu viongozi hao wachaguliwe hakuna maendeleo yoyote waliyoyafanya ndani ya jambo ambalo linawafanya wananchi hao kukosa imani nao.

Walieleza kuwa katika kipindi cha kampeni viongozi hao waliwaahidi mambo mbali mbali ambayo watayafanya ikiwemo kutatua tatizo la barabara za ndani ambazo zipo katika hali mbaya, lakini hadi hivi sasa hakuna hatua yoyote iliyofikia ya utengenezaji wa barabara hizo.

"Tuliwaambia hapa petu tunatatizo la barabara ambazo zipo nne za njia za ndani zinazohitaji matengenezo ikiwemo barabara inayokwenda skuli ya msingi Kibondeni lakini hadi hivi sasa hakuna hatua yoyote waliyoifanya viongozi wate hao mpaka hivi sasa,"walieleza wananchi hao.

Walisema wanashangazwa kuona baadhi ya majimbo mengine yakiwa na maendeleo wakati jimbo lao likiwa nyuma kimaendeleo.

Walisema wananchi hususan kinamama wajawazito hupata shida wakati wa kutaka kujifungua kutokana na ubovu wa barabara wanapo huhitaji kwenda hospitali kwa kujifungua.

Katika hatua nyengine wananchi wao wameiomba Baraza la Manispaa kufanya jitihada za kiliondosha jaa liliopo Jumbi ili kuepukana na maradhi yanayoweza kusababishwa na jaa hilo.

Mmoja wa wananchi hao, Hidaya Bilali Shomari, alisema kuwepo kwa jaa hilo katika maeneo hayo kumekuwa kukisababisha wananchi kupata homa za mara kwa mara pamoja na maradhi ya matumbo ya kuharisha.

Alisema njia ambazo wananchi hutumia ili kuepukana na maradhi hayo wamekuwa wakichukua tahadhari mbali mbali za kujikinga na maradhi hayo.

Hivyo aliiomba serikali kuliondosha jaa hilo kwenye maeneo hayo ambayo makaazi ya watu na kulihamishia katika maeneo mengine ambapo aliongeza kuwa kipindi hichi cha masika limekuwa kero kubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.