Habari za Punde

KADA YA UDAKTARI IREJESHEWE HESHIMA

Wanaojiita madaktari bila sifa wapondwa

Na Mwanajuma Abdi

WAZIRI wa Afya Juma Duni Haji ameitaka Bodi ya Baraza la Madaktari kufanya kazi zao kwa kufuata maadili na sheria ili waweze kurejesha heshima ya kada hiyo.

Kauli hiyo aliitoa jana, wakati akizindua Bodi hiyo katika ukumbi wa Wizara ya Afya, Mnazi Mmoja mjini Zanzibar.

Bodi ya Baraza hilo ni Mwenyekiti wake Dk. Malik Abdullah Juma na wajumbe ni Dk. Shaaban Issa Mohamed, Dk. Semeni Shaaban Mohammed, Dk. Hakim Gharib Bilal, Dk. Yunus Pandu Buyu, Dk. Omar Saleh Omar, Omar Juma Khatib, Dk. Faiza Kassim Suleiman na Fatma Saleh Amour.

Waziri Duni alisema Bodi hiyo ina kazi kubwa ya kusimamia maadili ili kuipa heshima taaluma hiyo, ambapo huko nyuma imepoteza muelekeo kutokana kuvujisha siri za wagonjwa na baadhi ya watu kujiita madaktari wakati hawana sifa hizo.

Alisema taaluma yeyote isiyokuwa na maadili haiwezi kufika mbali, ambapo alitoa mfano fani ya ualimu nayo imepoteza muelekeo kutokana na baadhi ya walimu kufanya mapenzi na wanafunzi hadi kuwapa ujauzito.

Waziri Duni alisema si vyema kila mtu akajiita daktari wakati hana sifa hiyo kwa vile mwili wa binadamu si sawa na kuchinja mbuzi na ng’ombe.

Aliongeza kusema kumekuwa na wimbi kubwa la watu kijiita madaktari wakati hawana sifa hizo, lakini Bodi hiyo itafuta kasoro hizo zilizokuwa zinajitokeza huko nyuma.

Aidha alisema kuwa Bodi hiyo ina jukumu kubwa la kuhakikisha siri za wagonjwa hazitolewi kwani ni moja ya jambo lenye kukiuka maadili ya kazi zao.

Alifahamisha kuwa, Baraza lililojiuzulu lilikuwa na madai mbali mbali ikiwemo kuingiliwa uhuru katika utendaji ambapo aliahidi kuwa hilo halitotokea kama ilivyokuwa Bodi ililopita labda wawe na mambo yao mengine.

Hata hivyo aliwataka wafanye kazi vizuri bila ya woga na kamwe uongozi hautoingiliwa na watafuata sheria na kanuni zilizopo.

Aidha alifahamisha kuwa, utendaji wa kazi uanze mara moja na wasisubiri hadi mabadiliko ya sheria, ambapo muda utakapofika wa marekebisho hayo yatafanywa huku utekelezaji ukiendelea.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Madaktari, Dk. Malik Abdullah alisema uteuzi wa Baraza hilo unafanyika kila muda wa miaka mitatu.

Alieleza mambo ya kuzingatiwa ni pamoja na kufanyiwa marekebisho ya baadhi ya vipengele vilivyokuwemo katika sheria pamoja na kuomba wasiingiliwe katika utendaji wao wa kazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.