KAMISHNA wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa amewataka wananchi wa Wilaya ya Magharibi kuimarisha Kamati za Ulinzi, Usalama na Ustawi wa jamii ili kupunguza kero mbali mbali za uhalifu katika maeneo yao wanayoishi.
Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na Kamati za Ulinzi, Usalama na Ustawi wa jamii huko Fumba, Kombeni, Nyamanzi, Bweleo, Dimani na Shakani Wilaya ya Magharibi Unguja.
Alisema Kamati za Ulinzi na Ustawi wa jamii ni muhimili muhimu wa kutatua kero za Uhalifu kwani licha ya uhalifu kupungua kwa kipindi cha mwaka 2010 bado baadhi ya maeneo kero zipo na zinahitaji kupatiwa ufumbuzi kupitia kamati hizo.
Alibainisha kwamba iwapo Kamati hizo zitafanya vikao mara kwa mara, kupeana taarifa na kuzipatia ufumbuzi taarifa hizo, vitendo vya kihalifu vinaweza kutoweka lakini kama wataendelea kuoneana muhali miongoni mwao watajikuta wakiishi katika hali ya wasi wasi.
“Iwapo Kamati hizi zitafanya vikao mara kwa mara, kwa kupeana taarifa bila shaka mutapata ufumbuzi wa matatizo yenu na huu ndio msingi wa kuanzishwa kwa Kamati za Ulinzi, Usalama na Ustawi wa jamii ngazi ya Shehia ikiwa ni njia moja wapo ya kudumisha mashirikiano yetu kati ya Polisi na jamii kupitia sera ya Polisi Jamii/Ulinzi Shirikishi”, Alisisitiza Kamishna.
Alisema Polisi Jamii ni Sera kama zilivyo sera za vyama na taasisi nyengine hivyo sera hiyo ni sera ya Majeshi yote duniani inayotilia mkazo ushirikishwaji wa jamii katika kutatua kero za Uhalifu, kwani bila ya kuwepo mashirikiano ya dhati kati ya pande hizo mbili suala la Usalama litabakia kuwa ndoto.
“Jamani nchi nyingi duniani zimefanikiwa kupunguza Uhalifu kupitia Sera ya Polisi Jamii kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita lakini hapa kwetu sera hii imeanza kusikika masikioni mwetu mwaka 2006, hata hivyo hatujachelewa ni wakati sasa kila mtu kwa nafasi yake ahakikishe kuwa ana jukumu la kudumisha ulinzi katika eneo lake’’, alisema Kamishna.
Alitolea mfano Shehia za Kwaalinato, Miembeni, Makadara na Mkele ambako kulikuwa na kero mbali mbali za Uhalifu lakini baada ya wananchi hao kuunda Kamati za Ulinzi, Usalama na Ustawi wa jamii na kukaa vikao waliweza kupata ufumbuzi wa matatizo yao na kuwafanya wananchi hao kuishi kwa usalama na amani.
Kamishna Mussa alisema kwamba Zanzibar yenye amani bila Uhalifu inawezekana iwapo tu wananchi watakuwa na nia ya dhati kwa kuwa mifano ya maeneo korofi ya Uhalifu yapo na yamefanikiwa kupunguza Uhalifu kupitia Kamati za Ulinzi, Usalama na Usatwi wa jamii kwa kuunda vikundi vya Ulinzi Shirikishi.
Alisema Polisi Jamii/Ulinzi Shirikishi ni Ushirikishwaji wa wananchi katika suala zima la kukabiliana na kero mbali mbali zilizomo ndani ya jamii yao inayowazunguka ili wananchi hao waweze kufanya shughuli zao za maendeleo kwa hali ya amani na usalama.
Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi, Usalama na Ustawi wa jamii Kwaalinato, Bw. Mussa Majura alitoa ushuhuda kwa wananchi hao kuwa katika Shehia yao ya Kwaalinato mwananchi wa kawaida alishindwa hata kupokea Simu akiwa nje ya nyumba yake kwa kuhofia kunyang’anywa na wajanja lakini walikaa pamoja kuunda Kamati za Ulinzi na vikundi vya Polisi Jamii na hivi sasa wananchi wanadiriki kuishi madirisha wazi.
“Niwaambieni ndugu zangu wa Fumba na Bweleo katika Shehia yetu kabla ya kuanzisha Polisi Jamii kila nyumba 10 basi nyumba nane(8) zilikatwa madirisha na wahalifu lakini katika kipindi hiki cha joto tumefika hatua kulala madirisha wazi bila kuibiwa, na hii yote inatokana na umoja wetu na ndio maana leo hii tumekuwa mfano wa kuigwa, tunamshukuru sana Kamishna Mussa kwa ushirikiano wake wa kutupeleka Bara kupata elimu hii ya ulinzi.”
Bwana Majura amezitaka Shehia zote ambazo hazijaunda vikundi vya Polisi Jamii/Ulinzi Shirikishi waanzishe mara moja kwani hakuna miujiza ya kupunguza Uhalifu bila ya wananchi wenyewe kushirikiana na Jeshi lao la Polisi.
Ziara hizo zilizofanywa na Kamishna wa Polisi Wilaya ya Magharibi ni mfululizo wa azma yake ya kuzitembelea Shehia zote za Unguja na Pemba kwa lengo la kujadiliana namna ya kukabiliana na Uhalifu, ambapo kwa hivi sasa ameshakamilisha ziara yake Wilaya ya Mjini Unguja.
No comments:
Post a Comment