Wanafunzi wa skuli za sekondari na msingi za jimbo la Magomeni wametakiwa kujiepusha na vishawishi vinavyokwenda kinyume na maadili, tamaa na anasa na kuelekeza nguvu zao katika kujipangia njia zinazoweza kuwasukuma katika kuendeleza masomo yao.
Ushauri huo umetolewa na Muakilishi wa jimbo la Magomeni Salmin Awadhi Salmin na Mbunge wa jimbo hilo Muhammed Amour Chombo wakati walipokuwa wakizungumza na walimu, wanafunzi na wazazi wa jimbo la Magomeni katika sherehe za kuwakabidhi sare wanafunzi 470 waliofanya vizuri katika mitihani yao ya darasa la saba, kumi na kumi mbili huko katika skuli ya secondari ya Sebleni.
Alisema kufaulu kwa hatua hiyo isiwe fahari kwao lakini iwe changamoto ya kuendeleza masomo yao kwa daraja nyengine na kufikia elimu za juu zaidi.
Aliwafahamisha wananfunzi hao kwamba vitendo vya anasa, utoro na ukosefu wa nidhamu ni mambo ambayo yanaweza kurejesha nyuma maendeleo yao.
`Hakuna uhodari wa akili pekee yake lakini nidhamu ni moja ya suala muhimu linalojenga hashima kubwa katika maendeleo ya binadamu hivyo lazima muendeleze masomo mkiwa na nidhamu ya kutosha` alisema Awadhi.
Nae mbunge wa jimbo hilo Muhammed Chombo amewasihi wanafunzi hao kutopoteza muda wao kwa kushughulikia mambo ambayo hayajawa tayari kwao kuyafanya na washughulikia elimu ambayo amabayo ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo yao.
`Najua wanaume mnajali kuowa na wanawake kuolewa lakini wakati huo kwenu bado shughulikieni elimu kwani wakati utakapowafikia hakuna atakayewazuia lakini hivi sasa wakati wake bado` alisema Chombo.
Aliwataka wazazi kuendelea kushirikiana vyema na walimu wa skuli kwa kuwajengea mazingira mazuri wanafunzi ili kuona wanaendelea vizuri katika masomo yao.
Mapema mwanafunzi Khamis Hassn akisoma risala kwa niaba ya wanafunzi wenzake 470 wakiwemo wanawake 243 waliokabidhiwa sare hizo zenye thamabi ya shilingi milioni tatu wanafunzi hao waliwapongeza viongozi hao kwa kuendelea na utaratibu wao wa kutoa sare kwa kila mwaka kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo yao.
Walisema kuwa utaratibu huo umekuwa ukiwapunguzia mzigo mkubwa baadhi ya wazee ambao vipato vyao vimekuwa vya chini kakabisa.
`Huu sio msaada mdogo na tunauthamini sana kwani sisi wengine wazee wetu hali zao hazisemeki hivyo kupata msaada huu ni kuwapunguzia mzigo mkubwa` alisema mwanafunzi huyo huku akishangiliwa na wanafunzi wezake.
Utaratibu wa kuwakabidhi fomu wanafunzi wa jimbo la Magomeni kwa wanafunzi wanaofaulu masomo yao ulianzishwa na uongozi wa jimbo la magomeni tangu mwaka 2000 utaratibu ambao umekuwa ukipongezwa na wazee na wazazi wengi wa jimbo hilo
No comments:
Post a Comment