Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu katika Wizara ya Nishati, Bi.Ziana Mlawa (Wa tatu kutoka kulia mstari wa nyuma) akiwa Katika picha ya pamoja na Wanafunzi aa Kike Kumi waliopata ufadhili aa masomo Katika masuala ya Nishati Endelevu kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja Wa Mataifa (UNDP) na Ubalozi wa Ireland.
Ni kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ubalozi wa Ireland 
Ufadhili huo ni utekelezaji wa Mpango Kazi wa mwaka 2018 wa Matumizi Bora ya Nishati
Mkurugenzi wa Utawala Wizara ya Nishati ashukuru UNDP na Ubalozi wa Ireland kwa ufadhili Wanafunzi 10 wa kike nchini wamepata ufadhili wa masomo katika masualaya Nishati Endelevu kupitia Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ubalozi wa Ireland katika mwaka wa fedha 2025/2026 ikiwa ni matokeo ya ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Nishati na UNDP katika kuwajengea uwezo Wanawake wa Tanzania katika masuala ya Nishati.
Kutolewa kwa ufadhili huo ni utekelezaji wa Mpango Kazi wa mwaka 2018 wa Matumizi Bora ya Nishati ambapo pamoja na masuala mengine, suala la kuwajengea uwezo wanawake katika masuala ya nishati limeainishwa.
Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza Wanafunzi hao jijini Dar es Salaam tarehe 24 Oktoba 2025, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Ziana Mlawa amesema kuwa kutolewa kwa ufadhili huo kunawawezesha Wanawake wa
Tanzania kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa mfumo wa nishati endelevu na rafiki kwa mazingira huku kukiwa na kiwango kidogo cha uzalishaji wa hewa ukaa.
Mlawa ameeleza kuwa, Serikali, kupitia Wizara ya Nishati, imeendelea kuwawezesha wanawake katika masomo ya nishati, hususan katika ngazi ya elimu ya juu.
Vilevile, kupitia ushirikiano na wadau wake mbalimbali wakiwemo Ubalozi wa Ireland na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), imeendelea kuweka kipaumbele katika uwekezaji wa upatikanaji wa elimu ya juu na masuala ya uongozi kwa wanawake.
Ameongeza kuwa, tangu kuanza kutolewa kwa ufadhili wa masomo katika sekta ya Nishati kupitia Mpango Kazi wa mwaka 2018 wa Matumizi Bora ya Nishati wanafunzi wa kike takriban 35 wamenufaika na ufadhili wa masomo katika mwaka 2023/2024 na 2024/2025.
Mlawa ameishukuru UNDP na Ubalozi wa Ireland kwa kutoa ufadhili huo wa masomo ambao mwaka huu unafikia ukomo wake huku akiwaomba kuendelea kutoa ufadhili wa masomo hayo ambayo ni muhimu katika ukuaji wa Sekta ya Nishati.
Pia amekishukuru Chuo cha DIT ambacho ndicho kitatoa mafunzo kwa wanafunzi waliofadhiliwa.
Mlawa pia amewapongeza Wanafunzi wa kike waliopata ufadhili akiahidi kuwa Wizara iko tayari kushirikiana nao, kuwasaidia na kuwapatia majukwaa ambapo mawazo yao na ubunifu wao utasikika na kuthaminiwa.
No comments:
Post a Comment