Habari za Punde

UDHAIFU, UBINAFSI SUMU YA MUUNGANO - RAZA

Na Ramadhan Makame

MFANYABIASHARA maarufu visiwani Zanzibar Mohammed Raza, amesema matatizo yanayojitokeza kwenye mchakato wa katiba mpya na masuala ya Muungano yanatokana na udhaifu wa watendaji wanaojali maslahi yao binafsi na kuliyumbisha taifa.

Raza alieleza hayo jana katika hoteli Grand Palace, iliyopo Malindi mjini hapa alipokuwa akitoa tathmini aliyoombwa kuitoa juu ya mchakato wa katiba na masuala ya Muungano.

Alisema watendaji wa ngazi za kati ndio wababaishaji wa mambo, ambapo wamekuwa na unafiki, tamaa, uchu na uroho wa madaraka hali inayosababisha kujitokeza kwa matatizo.

“Wakati mwengine tumekuwa tukiwalaumu Watazania bara mengine yanasababishwa na watendaji wetu kwa kuwa wanafiki na wasiojali maslahi ya wananchi”, alisema Raza.

Alisema viongozi wakuu wa nchi wana nia njema ya kuliongoza taifa hili kwa amani na utulivu, lakini uchu wa madaraka na unafiki wa watendaji umekuwa ukiliyumbisha taifa kwa kujali maslahi yao zaidi ya wananchi.

“Wananchi wa Zanzibar ni watulivu, wapenda amani wanaopenda kushirikiana na wasiopenda ugomvi, lakini matatizo yapo kwa hawa wasaidizi wa viongozi wa juu”,alisema Raza.

Raza alisema suala lililo mbele ya wananchi wa Zanzibar ni kusimama pamoja na kujenga hoja wakiongozwa na hadidu rejea ‘terms of reference’ kuwa Zanzibar nchi iliyokuwa huru kabla ya kuungana.

“Hili lazima tuliweke wazi na nimelisema kwa zaidi ya miaka 20, na wabunge wetu walielewe, Zanzibar ilikuwa nchi kamili kabla ya kuungana na wala tusikubali kuburuzwa”, alisema.

Alisema wakati wa wananchi kuwekewa ‘menu’ na kikundi cha watu 20 na kuambiwa haya ndio maamuzi umekwisha, bali washirikishwe kikamilifu katika kila lenye maslahi ya kujenga nchi.

Alisema ufike wakati Watanganyika na Wazanzibari wavumiliane na kila mmoja asione mzigo kwa mwenziwe na kusisitiza kuwa aandamwe mwenye kutaka kuvunja Muungano.

Alisema hata hivyo wakati utakapofika wa kijadili katiba wananchi waruhusiwe aina ya Muungano wanaoutaka na serikali wanazozitaka.

Raza amelezimika kuitisha mkutano huo akidai kuwa ameombwa kufanya hivyo na wananchi wa Zanzibar na hiyo imekuwa kawaida yake kila yanapotokezea masuala yanayolihusu taifa.

1 comment:

  1. Mzee Raza amezungumza lakini alitakiwa kusema uwazi kwamba ni vigumu nchi mbili kuungana kisiasa, ikiwa moja ina wananchi milioni moja na ya pili ina milioni 44, bila hile ndogo kutokumezwa kwa mfumo huu wa uungano uliopo hivi sasa. Muungano wa namna hii hakuna duniani. Rejea uangalie miungano mbali mbali duniani kama vile muungano wa USSR, Szechoslovakia, Yugoslavia, nakadhaika. Miungano hiyo yote imekufa na majina (USSR, Szechoslovakia, Yugoslavia, nk) yamekufa na nchi zote hizo zilizokuwa zinafanya miungano hiyo wamekuwa wanachama tena wa umoja wa mataifa. Zanzibar inahitajia kurudisha uwanachama wake wa umoja wa mataifa na baadae kuzungumza upya muungano wa kiuchumi, utamaduni na kadhalika kama vile ulivyo umoja wa ulaya ya magharibi. Nchi hizo zimeungana kwa kila aina ya ushirikiano isipokuwa hakuna nchi inayotaka kupoteza kiti chake katika umoja wa mataifa. Mipaka yao imfunguliwa na watu wanakiuka mipaka bila vitambulisho, lakini alama za mipaka inajulikana na kila nchi inamabalozi kati yao.Nakubaliana na wewe mzee Raza kwamba viongozi wetu ndio wenya matatizo na wabaya kwani wanaogopa na wana ubinafsi wa kuchunga maslahi yao tuu na sio maslahi ya wananchi wa Zanzibar. Kuwepo na kutokuwepo muungano wa namna hii ilivyo sasa inategemea uwamuzi wa wananchi.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.