Na Mwanajuma Abdi
JAMII imeshauriwa kudai risiti na waraka dhamana ‘guarantee’ ya kifaa watachonunua ili kukabiliana na wimbi la uingizaji wa bidhaa feki nchini.
Ushauri huo umetolewa jana, Naibu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Teknohama James Kilaba wakati akijibu hoja za washikiri warsha ya siku moja ya Mawasiliano ya Utangazaji, simu na Posta iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyofanyika hoteli ya Zanzibar Ocean View iliyopo Kilimani.
Alisema sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano iliyopitishwa nchini mwaka jana, imeainisha muuzaji kutoa waraka na mnunuzi ana haki ya kudai 'guarantee' pamoja na risiti katika kukabiliana na wimbi la baadhi ya wafanyabiashara kuingiza vitu feki nchini.
Alieleza kwa mfanyabiashara aliye makini hatokubali kupata hasara ya kuingiza vifaa feki kwa sababu waraka huo utambana pindi kinapotokea matatizo mnunuzi atakirejesha.
Kilaba alifahamisha kuwa, mchakato wa kujenga maabara ya kupimwa kwa vifaa feki umeanza ambapo katika mwaka mpya wa bajeti unatarajiwa kuanza ujenzi huo na itakuwa ya pekee katika ukanda wa Afrika.
Aidha alisema ili sheria hiyo iweze kutumika vizuri kanuni inaandaliwa, sambamba na kuweka vipengele vitavyopambana na wizi wa simu na masuala mengine yatazingatiwa.
Nae Ofisa kutoka Shirika la Posta, Saida Mohamed akitoa ufafanuzi alisema sheria hiyo italisaidia kuimarisha huduma za Posta, ambapo wateja wataweza kufuatwa majumbani, sambamba na kuweka mipango mizuri ya watu kuweza kutatuliwa matatizo yanapowafika likiwemo masuala ya kuunguliwa moto ili kufikiwa kwa haraka kwa gari la kuzimia moto na huduma za gari la wagonjwa.
Nao washiriki hao walishauri TCRA kutoa elimu kwa wananchi juu ya ununuzi wa simu za wizi kwa vile sheria hiyo inaweza kuwatia hatiani, sambamba na kuweka wazi juu ya udhibiti wa vifaa feki vinavyoingizwa nchini.
Mapema akifungua warsha hiyo, Katibu Mkuu wa Miundombinu na Mawasiliano, Dk. Vuai Iddi Lila alisema sheria hiyo itasaidia maendeleo makubwa katika sekta ya mawasiliano nchini kutokana na mabadiliko ya teknolojia yanayokwenda kwa haraka.
Akitoa mfano wa simu kwamba ina kazi nyingi ikiwemo kuwasiliana, kutuma fedha na baadhi yake zinapatikana mtandao wa internet jambo ambalo linasaidia katika kupata elimu, hivyo udhibiti ni muhimu katika masuala ya mawasiliano.
Aliongeza kusema kwamba, sheria hiyo itasaidia kukuza ushindani kwa makampuni ya mawasiliano pamoja na kutambuliwa mitaa yote kwa kuwekwa rikodi zake.
Akifunga warsha hiyo, Mkurugenzi wa Sheria wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Elizabeth Nzagi alisema TCRA ndio wasimamizi wa sheria hiyo lakini kwa upande wa utangazaji (Brodcasting), sheria hiyo haifanyi kazi Zanzibar kwa vile Tume ya Utangazaji ya Zanzibar itajitegemea wenyewe.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika suala la utangazaji wamekataa kuunganisha katika sheria hiyo ili kulinda tamaduni zao na maudhui yaliyokuwepo visiwani humo.
Aidha alieleza sheria hiyo imeeleza kwamba, ujenzi wa minara na busta za utangazaji zimeelekezwa kujengwa mbali na makaazi ya wananchi kwa vile kuna mionzi yake ina madhara kiafya.
No comments:
Post a Comment