Habari za Punde

DCMA YAKANUSHA KUFUNGA CHUO

Na Aboud Mahmoud

BAADA ya kuenea tetesi kuwa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi Zanzibar (DCMA) kimefungwa na kusitisha kutoa taaluma ya muziki, uongozi wake umeibuka na kukanusha taarifa hizo.

Baadhi ya walimu na wafanyakazi wa chuo hicho wameliambia gazeti hili kuwa, chuo kipo wazi na kinaendelea kutoa mafunzo kama kawaida.

Uongozi huo umeeleza kushangazwa na maneno yanayosambazwa mitaani kuwa chuo hicho kimefungwa na hakitoi mafunzo ya muziki, jambo ulilosema halina ukweli.

Wamesema ni kweli aliyekuwa Mkurugenzi wa chuo hicho Hilda Kiel ameondoka, lakini bado chuo kinafanya kazi ya kufundisha muziki kama kawaida.

"Nashangaa kusikia watu wanadai chuo kimefungwa na hakitoi tena taaluma, nataka niwatoe wasiwasi, chuo kipo wazi na kinafanya kazi kama kawaida", alisema Mohammed Matona mwalimu wa DCMA.

Mmoja wa wafanyakazi wa DCMA Halda Alkanaan, amesema kuwa tangu kuondoka kwa Mkurugenzi huyo Hilda Kiel, walimu na wafanyakazi wote wanaendelea na kazi zao ikiwemo ile ya kutoa taaluma kwa wanafunzi wanaojifunza ala mbalimbali za muziki.

Alisisitiza kuwa milango ya chuo hicho iko wazi kwa wale wote wanaotaka kujiunga kwa ajili ya kuchota utaalamu wa muziki, na kuwataka wasisite kufika kwa kujiandikisha.

Aidha Halda alisema mipango yote iliyopangwa tangu uongozi wa Mkurugenzi aliyeondoka inaendelea kutekelezwa ikiwemo ile ya kuandaa maonesho kwa wanafunzi yanayoandaliwa kila mwisho wa mwezi, na kusema onesho la mwezi huu linatarajiwa kufanyika leo chuoni hapo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.