Habari za Punde

KUELEKEA BAJETI YA SERIKALI: TUONDOKANE NA MATUMIZI YASIYOKUWA YA LAZIMA

Kutoka kwa Mdau

Kila siku wananchi wanazidi kuona hali ya maisha ikiendelea kuwa ngumu kwao na fursa nyingi zaidi kuendelea kuwa finyu. Ni ukweli usiopingika kuwa hali ya kiuchumi duniani imezidi kuwa ngumu hata kwenye mataifa makubwa ya ulaya na amerika pia. Hali ya ugumu wa maisha imeonekana vilevile katika nchi tajiri za kiarabu ambazo zina rasilimali kubwa sana ya mafuta.

Tumeshuhudia tawala kadhaa zikianguka na nyingine zikiendelea kuhangaika kutaka kubaki na huku wakubwa wa ulaya na amerika wakitafuta suluhu ya matatizo yao kwa kuvamia nchi nyingine kivita au kiuchumi. Sasa hivi mataifa makubwa yanafanya hima kupata rasilimali za Libya na zile nyingine hapo mashariki ya kati na kwingineko ili kurekebisha uchumi wa nchi zao.

 Hivi karibuni, tayari tumeshasikia kuwa vyombo vikubwa vya fedha duniani vinajiandaa kuzikopesha Misri na Tunisia mabilioni ya dola ili kukamilisha azma yao ya kumiliki uchumi wa nchi hizo. Nchi za Ureno na Ugiriki nazo ziko mbioni kupatiwa fedha na vyombo hivyo vikubwa vya fedha duniani ili kurekebisha uchumi wao.

Ni ukweli usiopingika kuwa wimbi hilo la matatizo ya uchumi wa dunia haliwezi kuziacha nchi zetu bila ya kuleta athari au kuzitikisa. Kwa mfano, tunaendelea kushuhudia ongezeko la gharama za maisha kwa kupanda kwa bei za mafuta na vyakula. Bei ya mafuta katika soko la Dunia hadi jana Ijumaa ya 20 Mei ilikuwa ni $99.49 kwa pipa ikiwa ni ongezeko la 0.12% kwa bei iliyopita. Na inakadiriwa kwa tarehe kama hii mwakani bei ya pipa la mafuta katika soko la dunia itafikia zaidi ya $114. Kwa mantiki hiyo, hali ya ugumu wa maisha kwa wananchi wetu tuitegemee kuongezeka kila siku kama hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo hilo hazitachukuliwa.

Kwa kawaida, wananchi wanategemea kuwa ni lazima serikali itimize majukumu yake kwa kutumia kodi mbalimbali zinazokusanywa kutoka kwa wananchi na mambo mengine. Na kadri hali ya uchumi na kupanda kwa gharama za maisha kunavyoongezeka, uwezo wa mwananchi wa kawaida wa kujikimu hupungua sanjari na kuongezeka umasikini. Hivyo basi, serikali inawajibu wa kuangalia kwa karibu na uangalifu matumizi ya kodi za wananchi na kurekebisha yale maeneo yote ambayo yataongeza mzigo kwa wananchi hasa matumizi yasiyo ya lazima.

Kwa mfano, nina uhakika matumizi ya magari ya serikali kwa shughuli binafsi ni mzigo ambao unabebwa na walipa kodi bila ya ridhaa yao. Kwa siku, kwa wiki, kwa mwezi na mwaka, matumizi haya yana athari-hasi katika ustawi wa wananchi.

Aidha, utumishi na watumishi wa serikali wazingatie kufanya kazi zao kwa tija ilikuepusha matumizi mabaya ya rasilimali za wananchi. Uchelewaji, utegaji na uzembe mwengine katika maofisi ya serikali ni gharama ambayo pia inaongeza mzigo mkubwa kwa wananchi.

Maeneo mengine ambayo yana matumizi ambayo si ya lazima ni kwenye warsha, semina, makongamano, nk. Si kwamba hakuna tija katika mambo hayo, bali yale maeneo ambayo yatasababisha matumizi yasiyo ya muhimu yasitishwe mara moja. Iko haja ya makusudi kabisa kudhibiti matumizi haya na mengine kama hayo ambayo mbali na kuwa mzigo kwa wananchi pia yanapunguza uwezo wa serikali katika kutimiza malengo yake muhimu ya kuleta maendeleo kwa wananchi.

Vilevile, serikali ni vema ikawa makini zaidi kwa kudhibiti na kuimarisha vyanzo vya mapato yake na kupunguza kwa kiasi kikubwa misamaha ya kodi na kuziba mianya yote ya uvujifu wa mapato ya serikali. Mapato ya serikali ni mali ya wananchi kwahiyo wenye dhamana ya kuyadhibiti wanastahili kukumbushwa kuwa uadilifu na uaminifu ni wajibu wao mkubwa wa kwanza. Kitendo chochote cha ufujaji na ubadhirifu wa mapato hayo ni kinyume na matarajio ya wananchi waliotoa dhamana hiyo.

Wakati tukielekea katika kipindi cha bajeti ya serikali, ni vema bajeti zetu sasa zikaondokana na 'copy and paste' na 'business as usual' na kuangalia kwa undani zaidi ni nini kinaweza kuepukwa na kuwa na matumizi yatakayokuwa na tija. Si vema na wala si haki kwa serikali na maofisa wake kuendelea kudhani kwamba hali iliyopo sasa hivi ya ugumu wa maisha kwa wananchi ni jambo lisilohitaji uthubutu wa dhati wa kuliondoa. Utumishi wa serikali ni lazima uzingatie matakwa halisi ya mahitaji ya wananchi na wala si vinginevyo.

Wito wangu kuelekea bajeti inayokuja ni kwamba tuondokane na matumizi yasiyo ya lazima na bajeti zetu zilenge kupunguza ugumu wa hali ya maisha itakayoendelea kujitokeza ndani mwaka mpya wa fedha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.