Habari za Punde

UPASUAJI WA MACHO WAFANIKIWA ZANZIBAR

 Zaidi ya wagonjwa 1400 wapona

Na Juma Khamis

ZAIDI ya wagonjwa wa macho 1400 wamepona kabisa maradhi ya macho baada ya kufanyiwa upasuaji wa kisasa na daktari bingwa kutoka China, Dk. Jijiangdong katika kipindi cha miaka miwili kuanzia Mei, 2009.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Dk. Jijiangdong alisema upasuaji huo umefanikiwa baada ya serikali ya China kuipatia Zanzibar msaada wa vifaa vya kisasa vya upasuaji, ambavyo ndivyo vinavyotumiwa na nchi chache barani Ulaya.

Alisema vifaa hivyo ni pamoja na phacoemulsification system, Non Contact Tonometer, Ophthalmic A/B Scan, Auto-Refractor Keratometer, intraocular lens, viscoelastic agents na vifaa vyengine vya kisasa zaidi.

Alisema wagonjwa waliofanyiwa upasuaji sasa wanaweza kuona kama kawaida, ambapo asilimia 80-90 ni wagonjwa waliokuwa wakisumbuliwa na mtoto wa jicho.

Aidha alisema wengi wa wagonjwa ni watu wenye umri mkubwa lakini hata hivyo, ameweza kufanyika kazi kwa mafanikio makubwa baadhi ya kesi ambazo ziliwahusu watoto.

“Haya ni mafanikio makubwa, katika kipindi cha miaka miwili tumeweza kuwafanyika upasuaji wagonjwa 1400 ambao tayari walikuwa vipofu na sasa wanaweza kuona kama kawaida,” alisema Dk. Jijiangdong.

Aliwataka wananchi kufanya vipimo vya macho mara kwa mara ili kuweza kugundua kama wana mtoto wa jicho, au maradhi mengine ya macho yanayoweza kusababisha upofu kama hayakutibiwa mapema.

Jijiangdong ambae ni daktari wa kwanza kutumwa na serikali ya China kutoa huduma Zanzibar anatarajia kurejea nyumbani mwezi Juni baada ya mkataba wake wa kuhudumu kumalizika na serikali ya Zanzibar itatuma mtaalum mwengine wa macho kujaza nafasi.

Ataondoka huku wagonjwa wa macho wakipata faraja kubwa kutokana na ukaribu alionao kwa wagonjwa na jinsi alivyoweza kusaidia kupunguza athari za upofu ambazo zilikuwa zinawakabili wananchi wengi wa Zanzibar.

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.