Zanzibar ianzie kiswahili kuingia soko la Afrika Mashariki
Na Abdulla Mohammed Juma
WAKATI nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakifaidika na kuanzishwa kwa soko la pamoja la Afrika Mashariki, upande wa Zanzibar bado hakujaonekana fursa ya kunufaika na mfumo huo.
Kuna sababu nyingi zinazoifanya Zanzibar kuwa katika hali hiyo ilhali nayo ikihesabiwa sehemu ya Jumuiya hiyo kupitia uanachama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hiyo ni hasara na hatari kwa maendeleo na ustawi wa Zanzibar na watu wake, kwani huku nchi hiyo ikiendelea kutafuta muafaka na ndugu zake wa Tanzania Bara, wa namna bora ya kuwawezesha wananchi wa Unguja na Pemba kufaidika na EAC, haina budi hivi sasa kujiingiza hivyo hivyo kwani mambo yanaendelea.
Kwa kuanzia Zanzibar ambayo inakubalika kuwa ndiyo kitovu cha lugha ya kiswahili si Afrika Mashariki tu, bali duniani kote ni lazima itumie fursa hiyo kuwa kinara na kufaidika kupitia kiswahili hicho, badala ya kufunga mikono na kusubiri ambo yatatuke kupitia muungao ndio fursa kama hizo zitumiwe, hilo litakuwa kosa kubwa kwani mkiwa tayari neema zote zitakuwa zimeshachukuliwa na wengine na kamwe hamtoweza kurejesha nyuma wakati.
Kuna njia nyingi ambazo Zanzibar ikiwa itakuwa makini, kupitia kiswahili inaweza kufaidika katika nchi zote tano za Afrika Mashariki ambazo ukiondoa Tanzania bara zilizobakia ni 'zero' katika uelewa wa lugha hiyo.
Tukianzia na walimu wa lugha ya kiswahili hivi sasa wanahitajika katika skuli mbali mbali za nchi wanachama, ambazo zimo katika hatua za kuwafunza wananchi wake lugha hiyo iliyochaguliwa kuwa lugha ya Afrika Mashariki.
Soko hilo lipo kuazia skuli za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu, ambapo Zanzibar ina wahitimu wengi wa mafunzo ya ualimu wa lugha ya kiswahili kupitia Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni ambayo nayo iko chini ya SUZA.
Ni jambo linalosikitisha kuwa mbali ya kuwepo magwiji wa lugha ya kiswahili Zanzibar, hadi sasa viwango vya elimu vyao viko chini jambo ambalo linawakosesha fursa ya kutambuliwa kimataifa na wanabakia kuwa maarufu ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba na au kutumiwa kufanya kazi kwa malipo haba na Maprofesa na Madokta wa Kiswahili waliopo Tanzania Bara.
Kuna haja ya Serikali kupitia taasisi zake mbali mbali kama vile SUZA, kuweka mkakati maalum wa kuinua hadhi na viwango vya wataalamu wa kiswahili wa Zanzibar nao kupata PHD ili wawe Maprofesa vinginevyo si wao wala Zanzibar itayofaidika na utaalamu wao wa kiswahili.
Si vibaya hata Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ikawasaidia walimu wa kiswahili, pamoja na wanahabari kupitia Wizara husika ili waweze kuingia katika soko la ajira kwa kutumia kiswahili, kwani inaonekana maafisa wa Serikali ndiyo wenye kuelewa zaidi kuhusu suala hili kuliko wananchi kwa kuhudhuria vikao na kubakia na mambo kwenye makabati yao na vcwani mwao.
Kupitia watangazaji wa redio wa lugha ya kiswahili ambao wamejaa tele hapa Zanzibar, ni sehemu nyengine yenye soko katika nchi tano za Afrika Mashariki ambalo Zanzibar inaweza kufaidika nalo.
Watangazaji hao wanatafutwa kwa udi na uvumba na vituo lukuki vya redio vilivyofunguliwa nchini Burundi na Rwanda, baada ya kuingizwa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Miongoni mwa taasisi zenye nafasi kubwa ya kusaidia Wazanzibari kufaidika katika soko la Afrika Mashariki kupitia kiswahili, ni Idara inayosimamia Diaspora iliyo chini ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambapo itakuwa inajenga Ma-Diaspora zaidi katika nchi jirani ambao watatoa mchango mkubwa katika kuchangia maendeleo na uchumi wa Zanzibar, pamoja na kuitangaza Zanzibar.
Nyengine ni Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo ambayo katika kiswahili na habari ndiyo iliyopewa jukumu kitaifa kusimamia masuala haya na kuhakikisha yanaleta tija kwa wananchi na hatimaye nchi kwa jumla.
Ukiacha upande wa Serikali, Zanzibar pia ina Wabunge katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambao tabaan wanaelewa uwepo wa neema hizi na nyengine, lakini inashangaza kuona wapo kimya na wanayoyapata huko hubakia nayo kwenye nafsi na makabrasha yao.
Wabunge hawa ambao wananchi wengi wa Unguja na Pemba hawajui hata kama wapo, kwani hawajapita kujitambulisha jambo ambalo ni muhimu kwa vile wao hawakuchaguliwa majimboni na hawatakiwi kuwa na wasi wasi wa kuombwa kama wanavyokimbia wabunge wa nyumbani kwa vile wamechaguliwa a wananchi huko.
Wabunge hawa hawawezi kukimbia jukumu la kuwaelimisha Wazanzibari, kwai ni wao pekee wanaojua kinachoendelea na kupitishwa katika Jumuiya hiyo na uzuri zaidi ni kuwa hawapitwi na vikao.
Umefika wakati wa waliowachaguwa Wabunge hawa kuwakumbusha majukumu yao, vinginevyo miaka itakwisha mtachaguwa wengine faida haitoonekana.
Cha kushangaza ni kila unapotembelea nchi nyengine wanachama kama vile Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda, utaona ratiba katika magazeti ya nchi hizo ya Wabunge kutembelea maeneo mbali mbali kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na Jumuiya hiyo na vipi wanaweza kufaidika na fursa zilizopo.
Kama hilo halitoshi kila siku ya Alkhamis, Wabunge wa EAC wa Uganda wanafanya kipindi maalum cha kuzungumza na wananchi kupitia Televisheni kuhusiana na fursa zilizoko kwenye Jumuiya hiyo, kwa Zanzibar tokea kuripotiwa kuchagliwa kwao hakuna jambo la moja kwa moja waliloripotiwa kulifanya, wakati Zanzibar hivi sasa ina changamoto kubwa kwenye Jumuiya hiyo.
Taasisi nyengine zinazopata fursa ya kushiriki kwenye harakati za Jumuiya hiyo ni Chama cha Wanasheria wa Zanzibar, Mtandao wa Jumuiya Zisizo za Kiserikali Zanzibar (ANGOZA) na Jumuiya ya Wenye Viwanda na Wafanyabiashara Zanzibar, ambazo zinaelewa hatari inayoikabili Zanzibar kupitia makubaliano ya EAC.
Kama zinakereketwa na Zanzibar, Jumuiya hizi zingeunganisha nguvu zao na kuwaelimisha wananchi wa Zanzibar na kuwapa hata mbinu za kushiriki kufaidika na makubaliano yanayopitishwa na EAC, huku wakisubiri mustakbali wa muafaka na ndugu zao wa Tanzania Bara katika nafasi ya Zanzibar kwenye Jumuiya hiyo.
Taasisi za elimu ya juu za Zanzibar na vyombo vya habari, navyo vimeonekana kulala kabisa katika suala hili na kuliona kama ni la wanasiasa, huku wananchi wa Zanzibar wakikabiliwa na hatari ya kuingia katika mfumo ambao hawaujui ndeo wala sikio lenyewe na tabaan utawaathiri vibaya kiuchumi na kimaendeleo.
Ieleweke kuwa makubaliano yameshapitishwa na uhuru wa kufanya kazi katika nchi hizi bila vikwazo, bendera ipo na juzi wimbo wa Taifa ulizinduliwa hapo Mjini Dar es Salaam, sasa Zanzibar isijiamini kwamba itaendelea kubana, hilo halitawezekana kwani mambo yanafanywa kidogo kidogo yakifika mwisho ni kukubali na kufuata na kubakia 'tumevamiwa'.
Wazanzibari wanalazimika kujifikiria wenyewe katika kujenga mustakbali wa nchi yao kimaendeleo kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki na kamwe wasidhani kama kuna wa kuja kuwazindua au kusimamia maslahi yao kwenye Jumuiya hiyo ambapo hivi sasa kila mwanachama analia 'Mamaangu'.
No comments:
Post a Comment