WAFANYAKAZI 21 walipelekwa katika hospitali ya Chake Chake wakitokea Unguja wamekosa makazi ya kudumu baada ya kuwasili kisiwani Pemba.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, walisema tangu kuwasili kisiwani humo wamekuwa na tatizo la makaazi jambo ambalo ni kinyume na walivyoahidiwa.
Walifahamisha kabla ya kuwasili katika kituo hicho cha kazi waliahidiwa kupatiwa makaazi pamoja na huduma muhimu wanazopaswa kupewa.
Kutokana na hali hiyo wanalazimika kukaa chumba kimoja watu watano, ikizingatia hali ya mazingira si salama pamoja na nyumba hiyo kukosa huduma muhimu kama maji, umeme na choo jambo linalohatarisha afya zao.
“Tumeshanga kukuta haya tuliyoyakuta, baadhi ya hospitali za Pemba hazina nyumba za madaktari na sio kama hawalifahamu hili bali ni kuonesha kutowajali watendaji wake’’, walisema madaktari hao.
Walieleza kuwa imefikia hatua ya kuishi kwa wasamaria wema ambao wameguswa na tatizo la ukosefu wa nyumba za makaazi.
Walisema tangu wafike Pemba wameshahama mara nne ndani ya wiki moja hali inayowasababishia kupoteza mizigo yao sambamba na kuongezeka kwa gharama za matumizi hususan katika usafiri na chakula.
Walifahamisha kuwa licha ya kadhia hio na kukosa mapokezi mazuri kutoka wa wenyeji wao jambo linalowawia vigumu kufanya kazi zao, lakini bado wao wako tayari kufanya kazi na wamefurahi sana kupangiwa kazi Pemba.
Kwa upande wake Daktari dhamana wa hospitali ya Chake Chake, Sauda Kassim alikiri kupokea wahudumu hao wa afya na kusema hio ni faraja kwao kwani kilio cha muda mrefu cha kuwepo kwa uhaba kimepatiwa ufumbuzi.
Kuhusiana na suala kutopatiwa makaazi salama na ya kudumu kwa madaktari hao, alisema suala hilo wanalifanyia kazi na tayari wameshakaa na kamati ya wilaya kwa ajili ya utatuzi wa tatizo hilo.
Akizungumzia lawama waliyotupiwa ya kutowapokea vizuri na kutotoa mashirikiano ya karibu alisema wao wamewapa baraka zote na wapo nao bega kwa bega kuona kwamba hakuna tatizo wanalolipata wakiwa kazini na hata nje ya kazi.
Aliwataka wafanyakazi hao pamoja na matatizo waliyonayo wawe na subira kwani viongozi wao wako mbioni kuona tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa haraka.
No comments:
Post a Comment